Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema ujenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Nguzo za Zege cha TCPM Tabora kinachomilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania - TANESCO kupitia kampuni tanzu ya TCPM haukusudii kuathiri wala kudhoofisha uwekezaji wa sekta binafsi bali unaongeza uzalishaji wa nguzo za zege ili kukidhi mahitaji yaliyopo ambayo bado hayajatosheleza uhitaji wa nguzo hizo nchini.

Ameeleza hayo Februari 15, 2026 wakati akikagua mradi wa ujenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Nguzo za Zege cha TCPM Tabora, ambao umefikia asilimia 95 ya utekelezaji. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa nguzo za zege 120 kwa siku.

“Kiwanda hiki si tishio kwa sekta binafsi; kinakuja kuongeza nguvu katika kazi ambazo tayari zilikuwa zinafanywa na sekta binafsi ya kuzalisha nguzo za zege,” amesema Ndejembi.

Ndejembi amefafanua kuwa TANESCO kwa mwaka 2025 ilikuwa na uhitaji wa nguzo za zege 80,000, lakini zilizopatikana kupitia sekta binafsi ni nguzo 40,000 jambo lililosababisha kutokufikiwa kwa malengo ya mahitaji hayo.

Ameeleza kuwa pamoja na Serikali kujenga kiwanda hicho, bado kuna fursa kwa sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya nguzo za umeme kutokana na mpango wa TANESCO wa kuendelea kufanya maboresho kwa kuondoa nguzo za miti na kutumia nguzo za zege katika usambazaji wa umeme nchini.

Aidha, Ndejembi ameitaka Bodi na Menejimenti ya TANESCO kusimamia kikamilifu ukamilishaji wa kiwanda hicho ili mitambo itakapowashwa iweze kufanya kazi kwa ufanisi na ubora kulingana na mpango na malengo ya Kiwanda hicho.

Kadhalika, amewataka wafanyakazi waliopata ajira na watakaoajiriwa kutunza miundombinu na mitambo ya kiwanda hicho pamoja na kuweka mpango madhubuti na endelevu wa uendeshaji ili kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange amesema utekelezaji wa mradi wa kiwanda hicho cha nguzo za zege, kinachomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi bilioni 7.9.

Twange ameeleza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji, ambapo kufikia tarehe 20 Februari 2026 mkandarasi atakuwa amekamilisha kazi zote, tayari kwa kuanza uzalishaji.











Share To:

Post A Comment: