Tanga, Januari 21, 2026


Baada ya kustaafu nilishuhudia kitu kimoja, nilistaafu tarehe 1/7/2012 na baada ya wiki moja niliweza kupata Mafao yangu.


Hayo ni maneno ya Mzee Ndibalema Kisheru, mstaafu anayepokea pensheni kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Mzee Kisheru ambaye alitumikia nafasi mbalimbali serikali akimalizia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ameyasema hayo kwenye banda la PSSSF kwenye Maonesho ya Tano ya Wiki ya Huduma ya Fedha, ambayo yamefunguliwa rasmi leo Januari 21, 2026 na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) kwaniaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamisi Mussa Omar, kwenye viwanja vya Usagara jijini Tanga.

Aidha, mzee Kisheru amesema, “Miaka 13 imepita nimeendelea kupata Mafao yangu bila kusita” Alisisitiza.

Mstaafu mwingine ni Bi. Marjorie Peter Mdoe, ambaye aliishukurani Serikali na Mfuko kwa kuongeza kiwango cha malipo ya pensheni kwa wastaafu, ambapo kwa wale waliokuwa wakipokea kima cha chini cha sh. 100,000/= sasa wanapokea sh. 250,000/=.

“ Hii 100,000/= ilikuwa inatupa shida sana, lakini sikutegemea siku moja tungeweza kupata sh. 250,000/=. Kwahiyo sh. 100,000/= ninatumia na sh. 150,000/= naiweka kwa matatizo ya dharura kama ugonjwa. Kwa hiyo namuombea kwa Mungu huyu Mama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  kwa roho yake, mimi siwezi kumlipa lakini Mwenyezi Mungu atakwenda kumlipa, kwasababu binadamu huwezi kuwa mzuri kwa watu wote lakini kwangu mimi naona kanifanyia jambo zuri.” Alisema Bi. Marjorie Peter Mdoe.

Naye mwanachama wa PSSSF, Bw. Revocatus Josephat, ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera yeye amesema, uamuzi wa Serikali kupitia PSSSF kuanzisha huduma ya msaada wa mazishi ambapo inatoa sh. 500,000/= kwa familia ya mstaafu aliyefariki, na malipo ya mkupuo wa pensheni ya miezi 36 kwa wategemezi wanaotambuliwa na sheria ya mfuko, kama vile mjane/mgane na watoto wasiozidi umri wa miaka 21 wa mstaafu aliyefariki ni hatua nzuri na ya kupongezwa.

“ Hili ni fao zuri sana, kwasababu kifo hakitoi taarifa, majanga hayatoi taarifa, kwa hiyo wale watakaobaki watakuwa wanalia ndio, lakini pia watakuwa wanapongeza juhudi zako ulizofanya katika utumishi wa umma na utabaki na heshima ile ile. watasema ah.…. kweli huyu baba yetu/mama yetu alikuwa wa maana sana kwasababu juhudi zake tunaziona hata baada ya kifo chake.” Alisema Bw. Revocatus Josephat.

Akizungumzia mafanikio hayo ya Mfuko, Kaimu Afisa Mfawidhi PSSSF mkoa wa Tanga, Bw. Frederick Paschal,  alisema, matumizi ya TEHAMA yamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo ambapo huduma zote zinatolewa kupitia mtandao hali ambayo imepunguza mzunguko na kurahisisha mchakato wa madai na malipo ya pensheni na mafao mbalimbali.

“ Lakini pia Mfuko umeendelea kutekeleza dhamira ya dhati ya serikali ya kuhakikisha wastaafu wanaishi maisha ya stara kwa kuboresha pensheni zao, lakini kuanzisha mafao mapya ambayo yote yanalenga kuhakikisha mstaafu pamoja na wategemezi wake wanaishi maisha yenye furaha.” Alisema.

Mwisho

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: