Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amekagua ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba ya mlezi (matroni) katika Shule ya Msingi Segese, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Miradi hiyo ina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 490 na inalenga kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu kwa kundi hilo muhimu katika jamii.

Mhe. Mhita alifanya ukaguzi huo Januari 14, 2025, alipokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Kijiji cha Segese, Kata ya Segese.

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mkuu wa Mkoa aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, hususan kwa watoto wenye mahitaji maalum, akisema miradi hiyo itasaidia kuongeza usalama, malezi bora na mazingira rafiki ya kujifunzia kwa wanafunzi hao.

Ujenzi wa bweni la wanafunzi umegharamiwa kupitia fedha kutoka Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Msalala. Aidha, ujenzi wa uzio wa bweni hilo umefadhiliwa na Kampuni ya Bulyanhulu Gold Mine (BARRICK) kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa gharama ya shilingi milioni 238, huku ujenzi wa nyumba ya mlezi ukigharimu shilingi milioni 79.2.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Frank Nkinda ameshukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Elimu na kuwataka kuitunza na kuitumia vyema ili iweze kuwasaidia watoto hao wenye mahitaji maalum.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bi. Rose Manumba amesema ataendelea kuhakikisha miradi inasimamiwa vyema na kukamilika kwa wakati katika Halmashauri hiyo kusudi wananchi waweze kupata huduma bora na nzuri.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mkuu wa Shule ya Msingi Segese, Ndg. Alpha Matambo, amesema ujenzi wa majengo hayo utachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza usalama, uangalizi na malezi bora kwa watoto wenye mahitaji maalum, tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza ari ya wanafunzi kuhudhuria masomo na kuwapa wazazi na walezi imani ya kuwapeleka watoto wao shule katika mazingira salama na rafiki.










Share To:

Post A Comment: