KAMATI  ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imezipongeza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa utendaji kazi mzuri na mafanikio makubwa yanayoendelea kuonekana katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma.

Pongezi hizo zimetolewa Januari 16, 2026 bungeni jijini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo , Mhe. Deodatus Mwanyika, baada ya taasisi hizo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake katika kikao cha kamati hiyo.

Mhe.Mwanyika, ameongoza kikao cha kamati hiyo, pia amezitaka taasisi hizo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kutoa huduma bora na kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa wananchi ili kuchochea ushindani na ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara nchini.

Aidha, wajumbe wa kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha utendaji kazi wa NDC, TBS, BRELA na TIRDO ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuendelea kushughulikia changamoto zinazoibuka katika utoaji wa huduma kwa wananchi, pamoja na kusimamia miradi ya kimkakati ya maendeleo kwa weledi.

Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake, Mhe. Dennis Londo , Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Suleiman Serera, Menejimenti ya wizara na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara yake, ameihakikishia kamati hiyo kuwa wizara yake itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na kuahidi kushirikiana na kamati hiyo katika kuziwezesha taasisi hizi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kupata matokeo chanya yanayotarajiwa katika kuendeleza sekta ya viwanda na biashara na kukuza uchumi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, ameeleza kuwa shirika hilo limepiga hatua katika usimamizi wa miradi ya kimkakati na kielelezo, uendekezaji wa kongani za viwanda na uendeshaji wa kiwanda cha viuadudu na uzalishaji wa mbolea ya viuatilifu.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, Mkurugenzi mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi na Kaimu mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Ramson Mwilangali, wakiwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu ya taasisi zao kwa kamati hiyo, walibainisha kuwa taasisi zao zinalenga kutoa huduma bora kwa urahisi kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ili kukuza uchumi wa nchi.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Alex Sonna

Post A Comment: