Na Mwandishi Wetu

Maboresho ya huduma za afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni yameanza kuleta matokeo chanya baada ya idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa kwa siku kuongezeka kutoka wagonjwa 100 hadi kufikia 175.

Akizungumza kuhusu maboresho hayo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Handeni, Dkt.Hudi Muradi, amesema ongezeko hilo limetokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya hospitali, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuimarika kwa utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu.

Ameeleza kuwa kwa sasa huduma zote muhimu za uchunguzi wa magonjwa zinapatikana hospitalini hapo, huku huduma za kibingwa zikiendelea kutolewa muda wote, hatua inayowapunguzia wananchi gharama na usumbufu wa kufuata huduma hizo nje ya halmashauri.

Aidha, amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuimarisha imani ya wananchi kwa hospitali hiyo.

Mganga Mkuu huyo ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora na za uhakika kupitia utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ambao unalenga kuweka usawa katika upatikanaji wa huduma za afya kati ya wananchi wenye kipato kikubwa na wale wa kipato cha chini.

Amesisitiza kuwa hospitali itaendelea kuboresha huduma ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: