Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.CPA Amos Gabriel Makalla amemshukuru Rais wa Serikali ya Awamu ya sita Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kuboresha miundombinu ya Viwanja vya ndege vya Arusha na Manyara, lengo likiwa kupanua huduma za miruko ya ndege kwa saa 24 pamoja na kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa abiria hususani watalii.

CPA Makalla amesema hayo leo Oktoba 10, 2025, alipoungana na Menejimenti ya Uwanja wa Ndege Arusha pamoja na watoa huduma kwenye kiwanja hicho, ikiwa ni maadhimisho ya kilele cha Wiki ya huduma kwa Wateja iliyoanza 6 - 10 Oktoba, 2025 huku akiipongeza Menejimenti ya Uwanja huo, kwa kuendelea kutoa huduma bora sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege ambao umekuwa chachu ya ongezeko la watalii mkoani humo.

 "Dkt. Samia amekuwa na dhamira ya dhati ya kukuza utalii kwa kuhakikisha viwanja vinakuwa na miundombinu rafiki itakayowezesha kufanya kazi kwa saa 24 na kuruhusu kutua ndege kubwa, jambo ambalo linaimarisha sekta ya uchukuzi sambamba na kukuza utalii na uchumi wa Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla". Amefafanua CPA Makalla.

Ameongeza kuwa, licha ya Filamu ya Royal Tour kuvutia na kuongeza idadi ya watalii nchini, mkoa wa Arusha ni miongoni mwa eneo ambalo linanufaika kwa ongezeko kubwa la idadi ya watalii wanaoingia na kuwataka watoa huduma kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi kwa wageni na kuondoa kero kwa abiria.

Hata hivyo, amewataka watumishi na wadau wanaotoa huduma kwenye uwanja huo, kutambua kuwa wanayo dhamana ya kukuza utalii nchini kwa kufanya kazi kwa weledi ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wateja, huduma ambazo ndio chachu ya maendeleo ya uchumi na kukuza sekta ya utalii.

"Management ya Arusha Air Port imechangia kwa kiasi kikubwa Makampuni ya utalii kufanya kazi vizuri kwa ushindani na kuhakikisha watalii wanapata huduma bora na kwa wakati,  jambo ambalo linaongeza chachu ya maendeleeo na ukuzaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii nchini, hii inaonesha dhana kubwa ya kuwaamini vijana katika kazi" Amebainisha










Share To:

Post A Comment: