Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA Ashiraph Abdulkarim, amezindua rasmi wiki ya Huduma kwa wateja ili kuboresha huduma na kujenga upya imani kwa wafanyabiashara kwa kuhakikisha wanarejea katika biashara kwa usalama na utulivu.

Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 9, 2025 Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa wametoa msamaha wa kodi ya pango kwa miezi miwili kwa wamiliki wa maduka yaliyoharibiwa na moto ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kujipanga na kurejea katika shughuli zao za kibiashara.

“Tutatumia wiki hii kusikiliza changamoto za wafanyabiashara wetu na kuzifanyia kazi kwa haraka ili kuwezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao bila vikwazo”, ameeleza CPA. Abdulkarim

Amesema kuwa wametoa msamaha wa kodi ya miezi miwili kwa wafanyabiashara waliopoteza mali zao kwenye moto.

Aidha amesema kuwa maandalizi ya kuwapatia wafanyabiashara maeneo mapya ya biashara yamekamilika na biashara zilizoathirika zimeruhusiwa kuanza ujenzi upya wakati huu wa msamaha wa kodi.

CPA. Abdulkarim amesema kuwa na hiyo kwalengo la kuboresha mazingira ya soko, nafasi zaidi ya 400 za maegesho zimeandaliwa ili kupunguza msongamano na kurahisisha shughuli za biashara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Dar es Salaam Omary Yusuf Yenga, amesema uzinduzi wa soko jipya la Kariakoo ni mwanzo wa mapinduzi ya kibiashara ndani na nje ya nchi.

“Biashara haiwezi kustawi bila soko la kisasa , tunashukuru serikali ya Dkt. Samia kwa kuwa na soko lenye miundombinu imara na usalama wa uhakika jambo linalochochea ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema Yenga.

Hata hivyo ameupongeza juhudi za kuwawezesha wafanyabiashara kupitia semina za uongozi ambapo amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi na tija kazini.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo Severine Mushi, ameweka wazi kuwa ofisi rasmi za viongozi sasa zitakuwa ndani ya soko hilo hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji na kuboresha wa huduma kwa wateja.

“Tunataka kukuza uchumi wa taifa kupitia soko hili kutokana na changamoto zilizopita, tunapendekeza malipo ya kodi yaanze tena Januari ili kuwapa wafanyabiashara muda wa kujiimarisha,” ametoa rai Mushi.

Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wadogo (Wamachinga) Steven Lusinde, amehaidi ushirikiano wa karibu na shirika ya Masoko Kariakoo ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: