Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wametaarifiwa kuwa huduma zote za kibingwa zitapatikana ndani ya mkoa huo mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, hatua itakayopunguza mzigo wa wagonjwa kusafirishwa hadi Muhimbili na hospitali nyingine kubwa nje ya mkoa.

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema hayo Jumatatu, Septemba 22, 2025, alipohutubia wakazi wa Namtumbo katika mkutano wa kampeni.

“Hospitali ya Rufaa ya Mkoa tunakwenda kuimaliza ili huduma za kibingwa zipatikane ndani ya Mkoa wa Ruvuma. Hakuna tena kusafirisha watu kwenda Muhimbili au maeneo mengine. Huduma zote muhimu zitapatikana hapa hapa Ruvuma,” amesema Dkt. Samia.

Aidha, ameeleza kuwa serikali yake imefanikisha kuongeza upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 53 hadi 84, na kujenga vituo vitatu vya afya na zahanati sita ndani ya Jimbo la Namtumbo. Pia, imepanga kuongeza vituo vipya vya afya katika Litola na Mchomolo, pamoja na kupeleka magari ya wagonjwa ili kurahisisha huduma za dharura.

Dkt. Samia amesema maboresho hayo yanakusudia kupunguza masafa ya wananchi kufuata huduma za afya, kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana kwa wakati, na hatimaye kufanya mkoa wa Ruvuma kuwa kitovu cha huduma za kibingwa kwa wananchi wake.

Share To:

Post A Comment: