Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendeleza ruzuku za pembejeo na mbolea kwa wakulima, pamoja na ruzuku za chanjo kwa wafugaji ikiwa atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza taifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Septemba 21, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Dkt. Samia amesema serikali yake itaendelea kutekeleza mipango ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa kushirikiana na wananchi.
“Mbinga mmeongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, lakini ninajua haya ni matunda ya ruzuku inayotolewa na serikali, kwahiyo niwapongeze sana na niwaahidi kwamba serikali yenu itaendelea kutoa ruzuku za pembejeo, mbolea na mambo mengine, kwa wafugaji ruzuku ya chanjo,” amesema.
Dkt. Samia pia amebainisha kuwa serikali imeanzisha mpango maalum wa BBT Ugani, utakaowawezesha vijana kuajiriwa na kutoa huduma za ugani kwa wakulima, ili kuongeza ufanisi katika sekta ya kilimo.
“Lakini pia tutaendelea kutoa huduma za ugani na sasa hivi tuna mpango maalumu wa BBT Ugani ambapo vijana wataajiriwa kutoa huduma za ugani kwa wakulima,” amesema.
Akigusia masoko ya mazao, Dkt. Samia ameahidi kuwa serikali itaendelea kutafuta masoko yenye bei nzuri ili kuhakikisha wakulima wananufaika na jasho lao. Aidha, amesema changamoto za barabara zitapewa kipaumbele kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa mazao.
Post A Comment: