Mbunge mteule wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Chiku Issa, amewataka wanawake wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi ifikapo tarehe 29 Oktoba 2025 ili kumpigia kura Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika mkutano wa ndani na wanawake wa Jiji la Arusha, hususan wajasiriamali wa masoko ya Kilombero, Samunge na Soko Kuu, Chiku alisema wanawake wanayo nafasi kubwa ya kuhakikisha Dkt. Samia anaendelea kuongoza nchi kwa kipindi cha pili, kwa kuwa amedhihirisha dhamira ya mageuzi makubwa yatakayoanza ndani ya siku 100 za kwanza.

Mageuzi ya Kiuchumi

Chiku alibainisha kuwa kati ya vipaumbele vya awali, Dkt. Samia ameahidi kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mitaji ya wafanyabiashara wadogo na wa kati, jambo litakalowezesha akinamama wengi kuimarisha biashara zao na kuongeza kipato cha familia.

Sekta ya Afya

Mbunge huyo pia aligusia suala la afya, akieleza kuwa moja ya ahadi muhimu ni kuajiri wahudumu wapya wa afya 5,000 ndani ya siku 100 za kwanza za uongozi wake wa kipindi cha pili. Hatua hiyo inalenga kupunguza uhaba wa watumishi, kuongeza ufanisi na kuimarisha huduma za afya vijijini na mijini.

Mikopo kwa Wajasiriamali

Kuhusu mikopo, Chiku aliahidi kuwasogezea karibu elimu ya namna bora ya kupata na kurejesha mikopo, akisisitiza kuwa changamoto kubwa imekuwa ni uelewa mdogo wa akinamama kuhusu mchakato huo.

“Samia anapigania akinamama kwa vitendo, ni jukumu letu kuhakikisha tunampa kura ili aendelee kutekeleza mageuzi haya,” alisema Chiku.

Baadhi ya wanawake walioshiriki mkutano huo walieleza kuguswa na ahadi hizo, wakiahidi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa 29 Oktoba 2025 ili kumhakikishia ushindi Dkt. Samia.









Share To:

Post A Comment: