Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa mradi wa uchimbaji wa madini ya urani unaoendelea Namtumbo utakuwa nguzo ya maendeleo ya taifa, huku ukitoa ajira na kuchangia katika ongezeko kubwa la uzalishaji wa umeme nchini.
Akihutubia wananchi wa Namtumbo mkoani Ruvuma leo Jumatatu Septemba 22, 2025, Dkt. Samia amesema mradi huo hautaishia kwenye uchimbaji pekee bali utafungua milango ya matumizi ya urani kwa ajili ya nguvu za nyuklia, hatua itakayoongeza mchango wa Namtumbo kwenye maendeleo ya taifa.
“Kupitia mradi huu wa urani, siyo tu tutamaliza tatizo la ajira bali pia Namtumbo itatoa mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Dhamira yetu siyo kuchimba tu bali kufikia hatua ya kutumia urani kupitia nguvu za nyuklia kuzalisha umeme hapa Namtumbo,” amesema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa, ndani ya miaka mitano ijayo iwapo atapewa ridhaa ya kuongoza, serikali inalenga kuongeza mara dufu uzalishaji wa umeme nchini kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo jua, upepo, urani na maji.
Post A Comment: