Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi mpango kabambe wa kukiboresha kilimo cha parachichi nchini kwa kujenga vituo 50 vya kuhifadhia mazao hayo kwa teknolojia ya baridi, viwili kati yake vikijengwa wilayani Rungwe.

Dkt. Samia alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wakulima wanapata faida kubwa, kwani vituo hivyo vitakuwa na uwezo wa kuhifadhi parachichi hadi miezi mitatu, kusubiri bei ya soko la dunia kupanda kabla ya kuuzwa.

Aidha, aliahidi kuanzisha kongani za viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya parachichi, ambapo vijana watanufaika kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta, chakula cha mifugo na bidhaa nyingine kutokana na matunda yasiyokidhi soko la moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Dkt. Samia, serikali itatoa miche milioni moja bure kwa wakulima wapya na waliopo, sambamba na kuajiri maafisa ugani maalum kwa ajili ya zao la parachichi. Maafisa hao watasaidia wakulima kupima udongo, kupata mbolea sahihi na kutumia pembejeo ipasavyo ili kuongeza uzalishaji.

Amesema pia ruzuku za pembejeo na dawa zitaendelea kutolewa, ambapo tayari serikali imenunua dawa za thamani ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya wakulima wa parachichi.

“Wajibu wetu ni kukamata mkono wa mkulima iwe soko ni zuri au baya. Nimeamua kusimama nao bega kwa bega ili parachichi za Tanzania zipate ushindani mkubwa katika soko la dunia,” alisema Dkt. Samia.

Share To:

Post A Comment: