Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imeanza mchakato wa kuchukua mashamba na viwanda vya chai kutoka kwa wawekezaji waliokabidhiwa lakini wameshindwa kuviendeleza, ili kuyamilikisha kwa vyama vya ushirika na kuongeza tija kwa wananchi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 5, 2025 mjini Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, Dkt. Samia amesema kampuni za WATCO na Mohammed Enterprises zilizokabidhiwa mashamba na viwanda hivyo zimeshindwa kuviendesha ipasavyo, hali iliyosababisha kudorora kwa sekta ya chai na kuzorotesha maisha ya wakulima.

“Serikali tumeunda timu inayofanya tathmini ya mashamba na viwanda. Lengo letu ni kuyachukua na kuyamilikisha kwa vyama vya ushirika chini ya uongozi wa serikali. Lakini kabla ya hapo, tumewaelekeza wawekezaji waliopo walipe madeni yote ya wakulima na wafanyakazi wa viwanda. Serikali imeshawaunganisha na mabenki ili waweze kupata mikopo kulipa madeni hayo, na niwahakikishie, si muda mrefu madeni hayo yatalipwa,” amesema Dkt. Samia.

Aidha, akigeukia zao la parachichi, Dkt. Samia ametangaza mpango mkubwa wa uwekezaji katika Rungwe na mikoa mingine kwa kujenga vituo 50 vya kuhifadhia mazao ya parachichi na mbogamboga kwa kutumia teknolojia ya baridi.

“Tutajenga vituo viwili vya hifadhi ya parachichi hapa Rungwe, vitakavyoweza kuhifadhi mazao kwa zaidi ya miezi mitatu ili tusubiri bei za soko la dunia zipande. Pia tutajenga viwanda vidogo vya vijana chini ya mpango wa BBT kuongeza thamani ya parachichi, hasa zile zenye dosari, ili kuzalisha mafuta, chakula cha mifugo na bidhaa nyingine,” amesema.

Dkt. Samia pia alitangaza kuwa serikali itagawa miche milioni moja ya parachichi bure kwa wakulima wa sasa na wapya, pamoja na kuajiri maafisa ugani maalumu wa zao la parachichi kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalam kuanzia upimaji wa udongo hadi matumizi ya pembejeo.
Share To:

Post A Comment: