Mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema vijiji vitano vitahamishwa kupisha uhifadhi wa Hifadhi ya Ruaha kwa kuwa hifadhi hiyo ni chanzo kikuu cha maji yanayotumika kuzalisha umeme kwenye mabwawa ya Kidatu, Mtera na Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Ubaruku, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, leo tarehe 05 Septemba, 2025, Dkt. Samia amesema hatua hiyo inalenga kulinda uzalishaji wa umeme wa taifa na kuendeleza maendeleo yaliyopatikana kupitia usambazaji wa nishati vijijini.
“Hifadhi ya Ruaha ni muhimu sana kwa taifa zima. Tukiachia wananchi wakae na waharibu, basi mabwawa yote hayatakuwa na kazi ya kuzalisha umeme. Ndiyo maana vile vijiji vitano vimelazimika kuondoka,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, amebainisha kuwa serikali itakamilisha tathmini na kuhakikisha wananchi wote ambao hawajalipwa fidia wanalipwa kikamilifu.
Kuhusu changamoto ya ufinyu wa ardhi, Dkt. Samia serikali itanunua shamba la mwekezaji- Mbarali Estate na kuligawa kwa wananchi wa eneo hilo, akisisitiza kuwa ugawaji huo hautakuwa kwa masilahi ya viongozi bali wananchi wenyewe.
“Ninataka kusisitiza hapa kwa viongozi, shamba lile ni kwa ajili ya wananchi walioko kule, na si kwa ajili ya sisi viongozi,” amesema.
Post A Comment: