Na Munir Shemweta, WANMM MBARALI

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha Klinik Maalum ya Ardhi kwa ajili ya kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi katika maeneo ambayo mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki (LTIP) umetekelezwa.

Hatua hiyo ya Wizara ya Ardhi ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi kuhakikisha maeneo yaliyofanyiwa urasimishaji kupitia mradi wa LTIP wananchi wake wanamilikishwa kwa kupatiwa hati milki za ardhi.

Klinik hiyo maalum ya ardhi inafanyika Dar es Salaam katika manispaa ya Ilala, Dodoma eneo la Mpunguzi, Mbeya halmashauri ya Mbarali na mkoa wa Shinyanga katika halmashauri ya Kahama pamoja na Manispaa ya Shinyanga.

Kupitia klinik hiyo huduma mbalimbali zinatolewa kama vile umilikishaji ardhi wa papo kwa hapo kwa wamiliki waliokamilisha taratibu za umiliki, utoaji elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo wa utoaji huduma za ardhi kidigiti (e-Ardhi) na Usaidizi wa ufunguaji wa akaunti ya Mwananchi kwenye mfumo wa e-Ardhi.

Huduma nyingine ni Uhakiki na utambuzi wa viwanja vya Wananchi Uwandani, Utoaji wa namba ya malipo (control number) za ada mbalimbali za Serikali kwa ajili ya umilikishaji pamoja na Upokeaji, usikilizaji na utatuzi wa migogoro kiutawala.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Klink hiyo ya ardhi wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya katika kijiji cha Ubaruku tarehe 11 Agosti 2025, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Deogratius Kalimenze amesema, zoezi la urasimishaji katika halmashauri ya Mbarali lilihusisha umilikishaji viwanja 30,700 vilivyopangwa na kupimwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki (LTIP). Mradi huo ulifanyika Kata ya Rujewa, Ubaruku, Lugelele, Mabadaga, Igulusi, Kongoromswiswi na Madibira.

‘’Hapa Mbarali kazi iliyofanyika ni kubwa sana, zaidi ya viwanja 30,000 vimepangwa lakini kasi ya umilikishaji imekuwa na changamoto ndiyo maana wizara iliamua kusambaza wataalamu na kuweka klinik maalum ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu’’ amesema Kalimenze

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbarali Kanali Maulid Hassan Surumbu ametoa rai kwa watumishi wa Ardhi kuhakikisha wanaweka mipango na mikakati mahsusi viwanja vyote vilivyopangwa na kupimwa vinamilikishwa kwa wamiliki wake.

‘’Naomba niishukuru wizara ya ardhi na halmashauri ya wilaya ya Mabarali kwa kuratibu na kuendesha program maalum ya klinik ya ardhi kwa ufanisi mkubwa sana’’  amesema

Mmoja wa wakazi wa Igawa katika halmashauri ya Mbarali mkoa wa Mbeya Sheikh Haroun Ally Mkanyanga amefurahishwa na klinik maalum inayofanywa na wizara ya ardhi  katika maeneo mbalimbali nchini ambapo ametoa kwa wamiliki wa ardhi kuhakikishia wanafuatilia hati kwani zitawasadia katika masuala mbalimbali ikiwemo kuondoa migogoro ya ardhi.

Share To:

Post A Comment: