Mgombea urais kupitia Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu, amekuwa mgombea wa saba kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Bussungu alifika katika viwanja vya Tume hiyo leo saa 2:50 asubuhi, akiwa ameongozana na mgombea mwenza wake, Ali Makame Issa, pamoja na wapambe waliokuwa wakicheza ngoma ya Kigogo kwa shamrashamra kubwa.
Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Bussungu amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, ataongoza mapinduzi ya fikra miongoni mwa Watanzania sambamba na kuanzisha mageuzi ya kiteknolojia na kiuchumi nchini.
“Chama chetu kinakwenda kuleta mabadiliko makubwa ya fikra, mapinduzi ya teknolojia na uchumi, na mapinduzi ya njano katika fikra za wananchi,” amesema Bussungu.
Aidha ameongeza kuwa dhamira yake ni kuijenga jamii yenye usawa na kutumia “akili mnemba” katika kuendesha taifa, amesisitiza kuwa muda umefika kwa taifa kubadili mwelekeo wake wa fikra na maendeleo.
Hadi sasa, wagombea wengine waliokwisha kuchukua fomu ya kuwania urais ni pamoja na Samia Suluhu Hassan (CCM), Coaster Kibonde (Chama Makini), Doyo Hassan Doyo (NLD), Kunje Ngombare Mwiru (AAFP), Hassan Almas (NRA) na Twalib Kadege (UPDP).
Post A Comment: