Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuimarisha miundombinu ya barabara na kujenga soko pamoja na stendi mpya katika Wilaya ya Chemba, mkoa wa Dodoma, ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha maisha ya wananchi.

Akihutubia, Agosti 31, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jimboni Chemba, Dkt. Samia amesema changamoto kubwa iliyojitokeza kwa wananchi wa eneo hilo ni ubovu wa miundombinu ya barabara, hasa barabara ya Chemba–Soya yenye urefu wa kilomita 32.

“Barabara hii ni ya uchumi, ndiyo barabara ambayo kuna minada hufanyika kila Jumapili. Minada hii inaingiza kiasi kikubwa cha fedha ndani ya Halmashauri, lakini pia mifukoni mwa wafugaji na wafanyabiashara wadogo. Ni barabara muhimu na tunawaahidi kwamba tutaichukua na kuifanyia kazi. Inaweza isiishe mwaka huu wa fedha, lakini katika miaka ijayo tutaiweka kwa kiwango cha lami,” amesema Dkt. Samia.

Ameongeza kuwa mbali na Chemba–Soya, barabara nyingine tatu za ndani ya Wilaya ya Chemba zitaangaliwa uwezekano wa kukarabatiwa kupitia TARURA ili ziweze kupitika mwaka mzima, iwe ni kipindi cha mvua au kiangazi.

Share To:

Post A Comment: