Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo kwa ajili ya vijana wa Chamwino, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza Agosti 31, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Chamwino, mkoani Dodoma, Dkt. Samia amesema mashamba hayo yataletwa kwa mfano wa yale yaliyopo eneo la Chinangali ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo kwa vijana.
“Kwa upande wa kilimo ndugu zangu wa Chamwino tunakwenda kuanzisha mashamba makubwa hasa yale ya vijana, kama yale ambayo tumefanya pale Chinangali. Tutaanzisha mashamba hayo kwenye maeneo kadhaa ndani ya Jimbo letu la Chamwino ili vijana wetu wapate pahali pazuri pa kueleweka, waweze kufanya kazi zao na waweze kujitegemea,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Chamwino kuendeleza mshikamano na kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi ujao.
Post A Comment: