Msanii na mtangazaji maarufu nchini ambaye pia ni Balozi wa Kampeni ya Walete ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, ametembelea banda la TTCL katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Baba Levo ametumia nafasi hiyo kuzungumza na wateja, kuhamasisha matumizi ya huduma za TTCL na kueleza namna shirika hilo la umma lilivyo kiungo muhimu katika kuleta mapinduzi ya kidigitali nchini. Aidha, ametoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi za kuhakikisha TTCL inabaki kuwa mhimili wa mawasiliano salama na ya uhakika nchini.

Ziara hiyo imekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi na mashabiki waliokusanyika kwa wingi kushuhudia msanii huyo akiungana na watumishi wa TTCL kutoa elimu kuhusu huduma na bidhaa zinazotolewa na shirika hilo la kihistoria.

Akiwa katika mazungumzo na wataalamu wa TTCL, Baba Levo alieleza kufurahishwa kwake na maendeleo ya kiteknolojia yanayotekelezwa na shirika hilo, ikiwemo:Usambazaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,Uanzishaji wa Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao,Huduma ya intaneti ya kasi kwa wananchi

Huduma za simu na bidhaa za kisasa kama modemu, MiFi na huduma ya Faiba Mlangoni.

"TTCL ni alama ya taifa. Tunapaswa kujivunia kuwa na taasisi ya kizalendo inayohakikisha mawasiliano ya Watanzania yanakuwa salama, ya uhakika na ya gharama nafuu," alisema Baba Levo.

Kwa upande wake, Meneja wa Banda na Meneja Bidhaa wa TTCL, Bi. Janeth Maeda, alisema ujio wa Baba Levo unaashiria mshikamano kati ya taasisi za umma na wasanii wenye ushawishi mkubwa katika jamii.

"Tunamshukuru Baba Levo kwa kutenga muda kututembelea. Hii ni ishara kuwa jamii inatambua umuhimu wa TTCL kama taasisi ya umma inayotekeleza dhamira ya Serikali ya kuwafikishia Watanzania wote huduma bora za mawasiliano," alisema Bi. Maeda.

Maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo:
"Maonesho ya Biashara ya Kimataifa – Sabasaba, Fahari ya Tanzania," ambapo TTCL imeonesha kwa vitendo namna huduma zake zinavyounga mkono ajenda ya kidijitali ya taifa na uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, huku ikiwahakikishia Watanzania huduma bora, salama na nafuu.








Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: