Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, ameitaka Kamati ya Lishe ya Jiji la Tanga, kuhakikisha wanaifikia jamii kwa kuipatia elimu ya lishe bora ili kuweza kubadilisha hali ya lishe ya familia, na hivyo kupata matokeo yaliyokusudiwa. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati hiyo, Mhandisi Hamsini amesema suala la lishe bora linatakiwa kuanzia nyumbani hadi kwenye maeneo ya kazi, na amemtaka Afisa Lishe wa Jiji kutayarisha na kuweka vipeperushi vya kukumbushia umuhimu wa kuzingatia lishe bora katika mlo, na kuangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya uanzishaji wa bustani na ufugaji katika shule za bweni kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi. 

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa afua za lishe, Afisa Lishe wa Jiji la Tanga, Bi. Rehema Kirungi, amesema katika kipindi cha Julai 2024 - Juni 2025, shughuli mbalimbali za lishe zimefanyika ikiwemo ukusanyaji wa takwimu na uchambuzi kupitia nyenzo za kukusanyia taarifa za mwezi na kila robo mwaka. 

Kirungi amesema utambuzi wa hali ya lishe umefanyika kwa watoto 34,143 wa umri wa chini ya miaka mitano, ambapo watoto 57 (0.2 %) waligundulika na utapiamlo mkali na kufanyiwa matibabu. Amesema kitengo cha Lishe pia kimefanya usambazaji na ugawaji wa nyongeza ya matone ya Vitamini A, ambapo jumla ya watoto 42,433 (99%) wamefikiwa kati ya 42,660 waliotarajiwa.

Shughuli za lishe zinasimamiwa na kuratibiwa katika Idara ya Afya na utekelezaji wake unahusisha Idara mtambuka, pamoja na wadau mbalimbali wanao jishughulisha na afua za lishe.


Share To:

Post A Comment: