*Na Mwandishi wetu- RUKWA
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya, Mhe. Nyakia Ally Chirukile, amezindua rasmi mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa wajumbe wa kamati za wilaya hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuwa tayari kabla ya majanga kutokea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, yaliyofanyika tarehe 21 Julai, 2025 kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Menejimenti ya Maafa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Mhe. Chirukile amesema kuwa maafa kama maporomoko ya ardhi, mlipuko wa kipindupindu, radi na ajali za majini yameathiri jamii na uchumi wa wilaya hiyo.
> “Kuchukua hatua kabla ya majanga ni nafuu zaidi kuliko kushughulika na athari. Mafunzo haya ni nyenzo ya kuongeza ufanisi wetu katika kuzuia na kukabili majanga,” alisema Mhe. Chirukile.
Kwa upande wake, Kanali Selestine Masalamado kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Maafa, amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, na yana lengo la kuwawezesha viongozi wa serikali za mitaa kuwa mstari wa mbele wakati wa dharura.
Naye mwakilishi wa UNDP, Bi. Clara Peter Maliwa, amepongeza Wilaya ya Sumbawanga kwa kujitoa kikamilifu kushiriki mafunzo hayo na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo ya kukabili majanga nchini.
Mafunzo haya yamewaleta pamoja wajumbe wa Kamati Elekezi ya Maafa ya Wilaya na Kamati ya Wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, wakiwa na lengo la kujifunza mbinu bora za kupanga, kukabili, na kurejesha hali baada ya majanga.
Post A Comment: