Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa kwa Serikali kupitia gawio lake kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Akizungumza Juni 17, 2025, mara baada ya kutembelea banda la Wizara hiyo katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma ambako yanafanyika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa, Mhe. Simbachawene alisema hatua hiyo inaonesha namna wizara hiyo na taasisi zake zilivyojikita katika uwajibikaji na ubunifu wa rasilimali.
“Maliasili mnafanya kazi kubwa, nawapongeza sana. Ndiyo maana mmeweza kutoa gawio kwenye mfuko mkuu wa serikali. Naamini mtaendelea kufanya hivyo. Ongezeni ubunifu hasa kwenye eneo la utalii kwa sababu tunafahamu kuwa utalii una fursa nyingi,” alisema Mhe. Simbachawene.
Katika ziara hiyo, Waziri huyo alipokea zawadi ya asali safi ya Misitu Honey inayozalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), mmoja wa taasisi zinazounda Wizara hiyo na ambaye tayari anashiriki kikamilifu kwenye maadhimisho hayo ya kitaifa.
TFS, kupitia banda lake maalum, limekuwa likitoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa, taratibu za ajira ndani ya taasisi hiyo, pamoja na matumizi ya mfumo wao wa kidijitali wa e-Misitu, unaolenga kuongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa taarifa kwa njia rahisi na ya mtandao.
Akizungumza katika banda hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Meneja wa Kitengo cha Rasilimali Watu wa TFS, Bahati Mtomaye, alisema wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata elimu na taarifa kuhusu shughuli na bidhaa za TFS.
“Miongoni mwa bidhaa zetu maarufu ni asali ya Misitu Honey, miche bora ya miti, na mbegu za miti ya aina mbalimbali. Lakini pia, vijana wanaotamani kujiunga na TFS au kupata taarifa zaidi kuhusu ajira na utumishi, huu ni wakati wao wa kufika hapa,” alisema Mtomaye.
Kaulimbiu ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu ni: “Himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji,” ambapo kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Juni 23, 2025.
Post A Comment: