Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Juni 18, 2025 ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa shule ya amali Mwamapalala, Itilima Mkoani Simiyu, akielekeza kuwa lengo la ujenzi wa shule hizo ni kuwafanya wahitimu kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Dkt. Samia akiweka jiwe la msingi katika shule hiyo kwaniaba ya shule nyingine 26 zinazojengwa Tanzania bara, amewashukuru pia wakazi wa Itilima na Simiyu kwa ujumla kwa kujitokeza kwao kwa wingi kwenye ziara yake, wananchi pia wakiahidi kwenda naye mpaka mwezi Oktoba, watakaposhiriki uchaguzi Mkuu na kumpigia kura za kishindo kutokana na maendeleo yanayoshuhudiwa Simiyu.

"Mwelekeo wa serikali ni kukuza zaidi elimu ya amali, kama mnavyojua tulikuwa na elimu yetu lakini mtoto akimaliza kidato cha nne anatoka hana la kufanya, anasubiri ajira lakini sasa tumeamua kubadili mwelekeo kiasi kwamba mtoto akimaliza kidato cha nne ana ujuzi unaomfanya aweze kujiajiri au kuajiriwa." Amesema Rais Samia.

Katika hotuba yake, Rais Samia amewarai wazazi na walezi Mkoani Simiyu kuendelea kutoa fursa za masomo kwa watoto wao ili waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika sekta ya elimu nchini ikiwemo ufunguzi wa matawi ya Vyuo vikuu kwenye mikoa mbalimbali pamoja na ujenzi wa shule.

Kulingana na Rais Samia, Tangu mwaka 2021 Wilaya ya Itilima imepata shule mpya za msingi 42, za Sekondari 31 suala ambalo limeufanya Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuwa na shule za msingi 606 kutoka 564 zilizokuwepo awali pamoja na Sekondari 183 kutoka 152 zilizokuwepo mwaka 2020.

Awali Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda amemueleza Rais Samia kuwa wahitimu wa shule hizo za amali mara baada ya kuhitimu kidato cha nne watapata vyeti vya kawaida vya baraza la mitihani la.oha na cheti cha ufundi na elimu ya Sekondari ya juu watasoma kwa miaka mitatu na kupata cheti cha Diploma na cheti cha baraza la mitihani, matarajio yakiwa ni kuanza kupokea wanafunzi katika shule hizo 26 mwezi Januari mwaka 2026.
Share To:

Post A Comment: