Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa Watanzania kulipa kodi na tozo mbalimbali, akieleza kuwa maendeleo yanayoshuhudiwa kote nchini yametokana na makusanyo ya kodi kwenye ngazi za Halmashauri na Taifa.

Rais Samia ameyaeleza hayo wakati wa Mkutano wake wa hadhara Wilayani Maswa Mkoani Simiyu leo Juni 18, 2025, ikiwa ni siku ya tano na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi Mkoani humo, akiipongeza pia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa makusanyo mazuri yaliyowezesha ufikiaji wa lengo.

Rais Samia pia amewataka wananchi wa Maswa kujiandaa na kuchangamkia fursa za miundombinu mbalimbali inayojengwa Wilayani humo ikiwemo ujio wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza ambapo kulingana na Shirika la Reli nchini, Kituo cha kushusha na kupakia mizigo cha SGR kitajengwa Wilayani humo.

"Kutakuwa na fursa za ajira na zabuni wakati wa ujenzi na vilevile tujipange namna tutakavyonufaika na huduma za reli pindi ujenzi utakapokamilika. Tuanze kujielekeza kwenye uzalishaji zaidi, kuongeza thamani na kuyafikia masoko ya mbali kwa kupitia usafiri nafuu wa SGR." Amesisitiza Rais Samia.

Rais Samia pia amewahakikishia wananchi wa Maswa na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuwa serikali yake itaendelea kuwawezesha wananchi kupitia uwekezaji unaofanywa kwenye Halmashauri za Mkoa huo, akiiagiza Halmashauri hiyo pia kuongeza eneo la uwekezaji kwaajili ya Kiwanda cha Chaki Maswa, kutokana na uzalishaji wake kutegemewa na Taifa kwa ujumla.

Share To:

Post A Comment: