Serikali imesema inalipa kipaumbele cha juu malipo kwa makandarasi wa ndani kama mkakati wa kuimarisha uchumi wa taifa na kuendeleza uwezo wa kitaalamu wa wazawa katika sekta ya ujenzi.

Akizungumza Jumapili Juni 8, 2025 mkoani Mwanza katika mjadala na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya ujenzi, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema tayari zaidi ya Shilingi bilioni 90 zimeshalipwa kwa makandarasi wa ndani kati ya deni la zaidi ya bilioni 260, lengo likiwa ni kuhakikisha fedha za miradi ya ujenzi zinazunguka ndani ya nchi.

“Makandarasi wetu wa ndani wakilipwa, uchumi wa nchi unaimarika kwa sababu hela inabaki ndani yetu wenyewe. Rais Samia amenipa maagizo rasmi kuwa kipaumbele cha kwanza kiwe kwa malipo ya makandarasi wetu wa ndani,” amesema Ulega.

Ameeleza kuwa katika muda mfupi tangu kuteuliwa kwake kuongoza Wizara hiyo, tayari wamelipa kiasi hicho kwa utaratibu wa awamu huku takriban Shilingi bilioni 186 zikiwa bado hazijalipwa. Hata hivyo, ametoa hakikisho kuwa serikali itaendelea kulipa madeni hayo hatua kwa hatua kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha.

“Fedha zikipatikana hata kama ni kidogo, cha kwanza ni kuwalipa makandarasi wa ndani. Tunafanya hivi kwa nia ya kulinda uchumi wetu, kuzuia kufilisika kwa makandarasi wetu, na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati,” amesisitiza.

Waziri huyo amebainisha kuwa, pamoja na changamoto ya madeni mapya kutokana na kazi zinazofanyika kila siku, serikali inajitahidi kuwa na mfumo thabiti wa kulipa madeni hayo bila kuathiri utekelezaji wa miradi mipya.

Kuhusu suala la kutumia wataalamu wa ndani, Ulega amesema serikali inafanya mabadiliko makubwa kuhakikisha wataalamu na kampuni za ndani yananufaika moja kwa moja na miradi ya ujenzi. Amesema mabadiliko haya ni maagizo ya moja kwa moja kutoka kwa Rais Samia ambaye amedhamiria kuhakikisha wazawa wanajengewa uwezo wa kufanya kazi kubwa kama za kimataifa.

Akitolea mfano, Waziri Ulega alisema mwaka 2023 wakati wa maafa ya mvua za El Niño na Kimbunga Hidaya, Rais Samia alitoa kibali cha Shilingi bilioni 562 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu iliyoharibika, ambapo zaidi ya bilioni 400 kati ya hizo zilipelekwa kwa makandarasi wa ndani kupitia mikataba 72 kati ya 82.

Vilevile, ameeleza kuwa serikali imefanya mabadiliko ya kanuni za ujenzi ambapo sasa miradi yote yenye thamani ya chini ya Shilingi bilioni 50 inapaswa kufanywa na makandarasi wa ndani pekee, huku miradi ya zaidi ya kiwango hicho ikigombewa na wageni kwa masharti ya kushirikisha makandarasi wa ndani.

“Sasa hivi wageni hawaruhusiwi kugombea kazi za chini ya bilioni 50. Aidha, tunatengeneza kanuni mpya zitakazowalazimisha wakandarasi wa nje kushirikiana na wa ndani katika kila mradi,” amefafanua.

Kwa mujibu wa Waziri Ulega, serikali inatarajia kuona mabadiliko haya yakileta matokeo chanya ya muda mrefu katika kukuza uwezo wa makandarasi wa ndani kiufundi, kifedha na kiteknolojia.

Share To:

Post A Comment: