Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali inatambua kuwa elimu ya amali ni msingi wa maendeleo, kwani inatoa ujuzi wa moja kwa moja kwa vijana kuwawezesha kuingia katika shughuli za Kiuchumi.

Waziri Mkenda ameeleza hayo Juni Mosi, 2025, akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya eneo lililotolewa na wananchi wa Kijiji cha Kichokochwe Wete Visiwani Pemba kwa ajili ya kujenga Skuli ya Ufundi, ambapo amewapongeza wananchi kwa hatua hiyo inayochochea maendeleo endelevu.

‘’Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania ameagiza tujenge shule za amali ufundi, kwa upande wa Zanzibar, shule moja itajengwa Wete Kojani na nyingine itajengwa Kusini Unguja. Vijana watakaomaliza skuli kidato cha Nne watapata cheti cha sekondari na cheti cha ufundi’’ alisema Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuboresha miondombinu ya elimu na kuongeza fursa za elimu ikiwemo mikopo ya elimu ya juu, ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata elimu bora itakayowakomboa kimaisha.









Share To:

Post A Comment: