Na Benny Mwaipaja, Abidjan
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kwa dhati na kuthamini ushirikiano wa karibu na wa kimkakati na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) uliochangia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya miundombinu, nishati, maji, kilimo, na ustawi wa kijamii.
Mhe. Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akitoa majumuisho ya uwakilishi wa Tanzania katika Mkutano wa 60 wa Baraza la Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mkutano wa 51 wa Baraza la Magavana wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF), iliyofanyika katika Hoteli ya Sofitel Ivoire, Abidjan, nchini CΓ΄te d’Ivoire.
Alisema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa na ongezeko kubwa la ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambapo hivi sasa Serikali inatekeleza miradi ya maendeleo ya kimkakati 25 ikiwemo 21 ya Serikali (Tanzania Bara na Zanzibar) na miradi 4 ni ya sekta binafsi katika sekta za miundombinu, nishati, usafirishaji, maji, usafi wa mazingira, pamoja na kilimo, yote kwa pamoja ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 3.54.
Mhe. Dkt. Nchemba aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa Barabara za Mzungumko jijini Dodoma, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma. ambayo kukamilika kwake kutaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini Tanzania.
“Kwa kuwa miradi hii inaendana na vipaumbele vya kitaifa na Ajenda ya Maendeleo ya 2063 ya Umoja wa Afrika pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Tanzania inatarajia kuendelea kushirikiana na AfDB kupitia mikakati ya ADF-17 na vyanzo vingine vya fedha ili kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu kwa taifa na ukanda wa Afrika kwa ujumla” alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa chini ya Mfuko wa Maendeleo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADF) mzunguko wa 17, Tanzania itaendelea kupata rasilimali fedha kwa kutumia mifumo mbalimbali ikiwemo dhamana za mkopo ili kusaidia miradi mikubwa ya miundombinu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Tanzania.
Akizungumzia kuhusu Rais Mteule mpya wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Sidi Quld Tah, alisema Rais huyo mpya wa AfDB si mgeni kwa Tanzania ambapo alimpongeza kwa ushindi wake na kwamba Tanzania itashirikiana naye kikamilifu kuhakikisha agenda za nchi za kuharakisha maendeleo yake zinafikiwa kama alivyofanya mtangulizi wake, Dkt. Akinumwi Adesina.
Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB, imetimiza miaka 60 tangu kuzishwa kwake ikiwa na wanachama 81 zikiwemo nchi 54 za Afrika na imekuwa ikitoa mchango mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi hizo, ikiwemo Tanzania.
Mkutano huo wa Mwaka wa AfDB ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Kamishna wa Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Katibu Msaidizi wa Baraza la Mawaziri, Bw. Fidelis Mkatte pamoja na maafisa wengine waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania
Post A Comment: