Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa takribani Shilingi Bilioni 41.6 kwaajili ya ujenzi wa shule za Sekondari za amali (ufundi) kwenye Mikoa 26 ya Tanzania bara, dhamira ikiwa ni kuhakikisha Wahitimu wanakuwa na uwezo wa kujitegemea.

Waziri Mchengerwa amebainisha hayo leo Jumatano Juni 18, 2025 wakati wa Ziara ya Rais Samia Mkoani Simiyu kwenye Wilaya ya Itilima, wakati wa uzinduzi wa shule ya Sekondari ya amali Mwamapalala, kwaniaba ya shule nyingine zilizopo kwenye Halmashauri 26 za Tanzania bara.

"Dhamira yako Mhe. Rais ni kuwawezesha vijana, wanafunzi watakaosoma kwenye shule hizi 26 kote nchini waweze kujitegemea baada ya kuhitimu masomo yao ya sekondari. Mradi huu ulitoa mwenyewe ikiwa ni dhamira yako na ndoto yako takribani shilingi bilioni 41.6, fedha hizi zimeenda kote nchini" Amesema.

Katika maelezo yake, Waziri Mchengerwa amesema shule hizo zinasimamiwa na TAMISEMI na Wizara ha Elimu ambapo kwa Itilima takribani Bilioni 1.6 imetumika kwaajili ya ujenzi wake, akiziagiza Halmashauri zote zenye miradi ya shule hii kutumia mapato yake ya ndani kujenga uzio kwenye shule hizo za Amali nchini.

Kulingana na Mhandisi wa Wilaya ya Itilima Abbas Kilumile, Ujenzi wa shule ya amali Mwamapalala umefikia asilimia 96, ukijumuisha majengo 13 ikiwemo madarasa nane, mabweni 4, karakana za useremala, uashi na ufundi bomba ambapo kwasasa karakana ya ufundi umeme ndiyo ipo katika ujenzi.

Share To:

Post A Comment: