Na Mwandishi Wetu, Lindi
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema serikali haitaongeza hata siku moja kwa mkandarasi ambaye atabainika ameshindwa kukamilisha mradi wa ujenzi aliopewa na serikali kwa sababu za uzembe.
Ulega ameyasema hayo mkoani Lindi wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa ukarabati wa miundombinu ya ujenzi katika mikoa ya Kusini kufuatia maelekezo aliyopewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya mvua kubwa zilizonyesha mwaka huu kuharibu barabara.
Waziri huyo amewaambia wakandarasi hao kuwa wakati mzuri wa kumaliza kazi zao ni huu kabla ya kuanza kwa mvua za vuli na kwamba hatarajii wananchi kuteseka tena wakati wa mvua hizo kwa sababu ya uzembe wa waliopewa kazi ya kujenga barabara na madaraja.
“Serikali imewaamini na kuwapa kazi ya ujenzi wa barabara na madaraja ya kudumu, hakikisheni mnakamilisha kwa ubora na wakati na hatutakubali kuona tena wananchi wakiteseka kama ilivyotokea mwaka jana na mwaka huu”, amesisitiza Ulega.
Katika ziara yake hiyo ya ukaguzi, Waziri Ulega aliwasilisha pia salamu maalumu za upendo kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa mkoa wa Lindi ambako kwa sasa, serikali yake inaendelea na ujenzi wa miradi mikubwa takribani 13 inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Mbunge huyo wa Jimbo la Mkurange amewataka makandarasi wanaojenga madaraja na barabara unganishi mkoani Lindi kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili ikamilike mapema mwezi Septemba kabla ya kuanza kwa mvua za vuli.
Ujenzi unaoendelea sasa katika barabara za Kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kusini unafuatia athari za mvua za El Nino na kimbunga Hidaya ambavyo kwa pamoja vilisababisha kukatika kwa barabara za Marendego-Nangurukuru-Lindi-Mingoyo, Kiranjeranje-Namichiga, Tingi-Kipatimo, Nangurukuru-Liwale na Liwale -Nachingwea.
Ili kuhakikisha kwamba kazi ya ujenzi inakwenda kwa kasi, Ulega amewataka wakandarasi kuongeza idadi ya wafanyakazi na muda wa kufanya kazi – bila kujali usiku na mchana, ili kazi iende kwa kasi na pia kusaidia vijana kupata riziki.
Waziri Ulega amekagua na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi wa madaraja ya Somanga Mtama (m 60), Mikereng’ende (m 40), Njega II Matandu (m 60), Miguruwe (m 39), Zinga (m 18).
Kuhusu barabara ya Nangurukuru-Liwale, Ulega amesema wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imetenga zaidi ya bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi wa tuta la barabara katika maeneo korofi ya Njinjo na Ngea katika barabara hiyo na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni.
Ameitaka TANRAOADS ifanye matengenezo ya mara kwa mara ya barabara hiyo ili iweze kupitika vipindi vyote na magari ya abiria yaendelee kutoa huduma bila ya kikwazo chochote na kupunguza muda wa safari kutoka siku nzima hadi saa 4 na hivyo kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo, ameeleza kuwa ujenzi wa daraja la Somanga Mtama (m 60) una nguzo 43 za kubebea daraja na kati ya hizo nguzo 41 zimekamilika na mradi umefika asilimia 42, ujenzi wa daraja la Kipwata (m 40) una nguzo 34 na zote zimekamilika kujengwa na mradi umefikia asilimia 40.9.
Pia, ujenzi wa daraja la Mikereng’ende (m 40) lenye nguzo 43 zote zimekamilika kujengwa na mradi umefikia asilimia 51.5 wakati ujenzi wa daraja la Miguruwe (m 39) lenye nguzo 34 ambapo kati ya hizo nguzo 33 tayari zimekamilika kujengwa na mradi umefikia asilimia 33 huku ujenzi wa daraja la Njenga II Matandu (m 60) umefikia asilimia 16.
Post A Comment: