Wananchi wilayani Karagwe mkoani Kagera wameeleza kunufaika na ujenzi wa barabara ya Nyakahanga-Nyabiyonza -Masheli ambapo kero ya usafiri iliyokuwepo imeondolewa baada ya matengenezo ya maeneo korofi.
Akiongea katika mahojiano maalum, Diwani wa Kata ya Nyakahanga, Mhe.Charles Beichumila ameeleza kuwa kipindi cha masika wananchi wa kata za Nyakahanga na Nyabiyonza walikuwa hawawezi kuwasiliana kutokana na hali mbaya ya barabara.
"Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wetu Mhe. Innocent Bashungwa kwa utatuzi wa kero hii ya muda mrefu maana kwa sasa barabara inapitika kwa kipindi chote cha mwaka", amesema Mhe. Beichumila.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA wilaya ya Karagwe, Mhandisi Kalimbula Malimi amesema kuwa kipaumbele katika matengenezo ya barabara hiyo yenye urefu wa Km 96 kilikuwa ni kuanza na maeneo korofi kwa kuweka tabaka la lami na kwamba hatua itakayofuata ni kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami.
"Tumeanza na maeneo korofi kwa kuweka tabaka la lami ambapo hadi sasa tayari Km 9.2 zimekamilika na wananchi wanapita bila usumbufu", amesema Mhandisi Kalimbula.
Kwa upande wake, Bw. Josam Pastory mkazi wa kata ya Nyakahanga ameeleza kuwa kero kubwa iliyokuwepo ni hasa kipindi cha masika ambapo akina mama walishindwa kufika hospitalini huku watoto wakishindwa kufika shuleni kwa urahisi.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Karagwe inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya usafiri na usafirishaji kwa urahisi.
Post A Comment: