Na Egidia Vedasto, Msumba Arusha.
Mawasiliano kati ya viongozi na wananchi wao yameonekana kuzorota hatua iliyopelekea Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude kukemea hali hiyo.
Akizungumza katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 cha Baraza la Madiwani Jijini Arusha, amesema si vema wananchi kupeleka kero mojamoja katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wakati kwa uraratibu walitakiwa kuanzia ngazi ya chini.
Aidha amewataka viongozi wakiwemo Wenyeviti wa mitaa, Afisa watendaji wa mitaa na kata pamoja na Madiwani kupenda kuwasikiliza wananchi malalamiko yao na kuyafanyia kazi.
"Hatua ya wananchi kutafuta msaada wa ufumbuzi wa changamoto zao, hii inaonyesha kuwa ushirikiano ni mdogo katika ngazi za chini, na hii sitaki ijirudie, nendeni mkawasikilize wananchi waliwaamini na wanawategemea" amesema Mkude.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngarenaro Doita Isaya amekiri ushirikiano kuwa mdogo kwa baadhi ya viongozi na wananchi katika kata zao.
Hata hivyo kutokana na kauli ya Mkuu wa wilaya kuonya juu ya mawasiliano hafifu, amewakumbusha Madiwani wenzake kuwasiliana mara kwa mara na wananchi wao ili kuaminika na kushughulikia changamoto katika maeneo yao pale zinajitokeza.
"Kuna baadhi ya viongozi kweli suala la mawasiliano ni changamoto, wananchi hawajui viongozi wao, na wengine wanajulikana lakini wako bize na maisha mengine, tubadilike" amefafanua Doita.
Post A Comment: