Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaosimamia masuala ya fedha na uchumi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (17th SCFEA), uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo Jijini Arusha, leo tarehe 20 Mei, 2025, ambapo amehimiza nchi wanachama kuimarisha zaidi utengamano wa kikanda ili kuharakisha maendeleo ya nchi hizo.
Mkutano huo, pamoja na masuala mengine, umejadili taarifa ya mashauriano ya kibajeti kuhusu viwango vya pamoja vya Ushuru wa Forodha vya Afrika Mashariki kwa mwaka 2025/26; kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaosimamia masuala ya Fedha na Uchumi (16th SCFEA); na kupokea na kujadili Taarifa ya Mkutano wa Kamati ya Kikanda ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, agenda nyingine ilikuwa kupokea na kujadili taarifa ya mkutano wa pamoja wa Kamati ya Kisekta ya Masuala ya Bajeti na Kamati Ndogo ya masuala ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; kupokea na kujadili taarifa ya Warsha ya 11 ya kikanda ya Masuala ya Usimamizi wa Fedha na Bajeti na kupokea na kujadili taarifa ya Mkutano wa 28 wa Kamati ya Masuala ya Fedha (MAC).
Vile vile, mkutano umepokea wasilisho la nchi wanachama kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi jumla, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa vigezo vya uchumi jumla vya mtangamano wa kikanda na vipaumbele vya bajeti kwa mwaka 2025/26 kutoka kwa nchi wanachama; kujadili dhima za bajeti za nchi wanachama kwa mwaka 2025/26; pamoja na kubuni kauli mbiu moja ya bajeti ya EAC.
Post A Comment: