WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kupelekewa taarifa kamili za wasimamizi na mshauri mwelekezi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne baada ya kushuhudia uzembe unaosababisha usumbufu zaidi barabarani kinyume na malengo ya mradi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi huo unaotoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Mwenge hadi Tegeta, sambamba na tawi la kutoka Mwenge hadi Ubungo, Ulega alieleza kushangazwa na jinsi wasimamizi na mshauri mwelekezi wa mradi huo wanavyoonekana kufumbia macho uzembe huo.
Mojawapo ya maeneo ambayo yalimkera waziri huyo jana ilikuwa ni katika eneo la Palm Beach, Upanga ambako alikuta shimo kubwa limechimbwa na mkandarasi, pasipo kukamilisha kwanza kazi ya muhimu zaidi katika maeneo ya awali kutoka Morocco hadi Mwenge hadi Kaunda.
“Mimi nimepita kukagua. Kazi ambazo nimeaminiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni za barabara na madaraja. Rais hapendi na hafurahishwi na msongamano mkubwa hapa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini. Hisia hizo hajawahi kuzificha,” alisema Waziri Ulega.
Ameongeza kuwa alipohoji sababu ya kuchimba eneo jipya kabla ya kukamilisha maeneo ya awali, alielezwa kuwa ni mkandarasi huyo huyo ambaye bado hajamaliza kazi sehemu ya mwanzo.
“Nini kimemfanya awe na haraka ya kuja kutifua huku wakati kule hajakamilisha? Hii ndiyo hoja yangu na ugomvi wangu hapa,” alisema.
Waziri Ulega amesema amebaini tatizo kubwa liko kwa upande wa wasimamizi wa mradi pamoja na Mshauri Elekezi.
“Hii ni barabara ya umma, si mali ya mkandarasi. Mkandarasi hawezi kuvamia na kuchimba kiholela. Hapa shida si mkandarasi peke yake, ni wasimamizi na mshauri elekezi,” alisema kwa msisitizo.
Post A Comment: