Na Mwandishi wetu- Dar es salaam 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amezindua miradi ya kiuchumi ambayo iko chini ya  Shirika lisilo la Kiserikali la Strategic Alternative Learning Technique (SALT), inayohudumiwa na vijana wenye changamoto za ufahamu.

Mhe. Nderiananga alifanya uzinduzi huo Jijini Dar es Salaam kwa miradi ambayo ni pamoja na  Salt Special Supermarket, Mgahawa na Bakery itakayohudumiwa na vijana wenye ulemavu wa ufahamu huku akisema jumla ya vijana na Watoto 83 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutoa huduma kwa wananchi hatua itakayowasaidia kujipatia kipato chao na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Aidha, Mhe. Nderiananga aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ikiwemo elimu, kujiwezesha kiuchumi na kusaidia mashirika yanayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake  ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa fedha kwa watu wenye ulemavu ili wafanye kazi zao vizuri. Nimefurahi kuona Shirika hili la SALT linafanya kazi zake kwa ubunifu kwa kuwafundisha stadi za kazi na ubunifu wa mavazi,” alisema Mhe. Nderiananga.

Vilevile, alifafanua kwamba ikiwa  kila mmoja atafanya kwa nafasi yake katika kuwawezesha watu wenye ulemavu itaongeza chachu kwao kujituma kufanya kazi kwani vipaji na uwezo wao utatambulika na kuungwa mkono hali itakayoongeza uzalishaji katika Nchi.

“Nitoe wito tuendelee kuliunga mkono Shirika hili na mengine yanayowasaidia watu wenye ulemavu wa aina zote kwani yanafanya kazi kubwa hivyo viongozi wetu wa Serikali za Mitaa tuyapokee mashirika haya na kuwapa ushirikiano kwa manufaa ya Taifa letu.

Aidha alibainisha kwamba watu wenye ulemavu wanahitaji fursa bila kunyanyapaliwa huku akiwataka wazazi na walezi kutosikiliza maneno ya kukatisha tamaa na badala yake wawaamini watoto wao kuwa wana uwezo wa kipekee.

Aliwahimiza  wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kutumia fursa za mafunzo yanayotolewa katika taasisi mbalimbali ili kuwajengea Watoto kujiamini kuwa wanaweza na wanamchango katika jamii.

“Baadhi ya mafunzo yanayotolewa na SALT ni pamoja na uokaji, mapishi, mitindo ya mavazi na wahudumu katika migahawa hatua inayowajengea ujuzi wa kujipatia kipato ili kuendesha maisha hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Strategic Alternative Learning Technique (SALT), Bi. Rebeca Lebi alieleza kuwa Shirika hilo lilianza mwaka 2019 kwa lengo la kuwasaidia watoto na vijana wenye changamoto za ufahamu ambazo ni  Usonji (Autistic Spectrum Disoder), Down syndrome, Mtindio wa ubongo (Cerebral Palsy ), Ulemavu wa akili (Intellectual Impairment) , Kifafa kikali (Severe epilepsy) na changamoto zote zinazohusiana na ulemavu wa ubongo na ufahamu.

Awali akisoma risala  Meneja wa Operesheni kutoka Shirika la SALT, Bi. Jasmine Omary Iddy alisema SALT, ilianzisha chuo cha ufundi na uzalishaji (Vocational training and production) ikiwa na malengo ya kumuandaa kijana mwenye changamoto za ulemavu wa ufahamu kuweza kuwa mzalishaji  kupitia mpango wa Viwanda  10 ambavyo vitazalisha bidhaa tofauti, kama vile sabuni za kuogea, shampoo, mafuta ya kupaka, vitambaa vya batiki,  mikate na ufugaji wa samaki, kuku pamoja na bustani za mbogamboga.

“Kituo hiki kilianzishwa kwa lengo la kuwawezesha vijana wenye changamoto za kiakili na ufahamu kupata stadi za kazi, stadi za maisha na mazingira salama ya kujifunza na kushiriki katika shughuli za kiuchumi. Lengo letu kuu ni kuwapatia fursa ya kujitegemea, kuongeza thamani katika maisha yao na kupunguza utegemezi kwa familia au jamii,” alieleza Meneja huyo.

MWISHO

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: