Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Erasto Mpete amewataka wanafunzi wa kidato cha sita wanaoingia kwenye chumba cha mtihani kwenda kufanya mitihani yao kwa kujiamini na kupata matokeo mazuri kwa kuwa hakuna zawadi nzuri ya mtoto kwa mzazi zaidi ya kufaulu na kufanya vizuri kwenye mitihani.
Mpete ametoa agizo hilo mapema mara baada ya kuwatembelea na kuzungumza na wanafunzi wanaofanya mitihani katika shule ya sekondari Yakobi iliyopo katika halmashauri ya mji wa Njombe ili kuwatia moyo wanapofanya mitihani yao.
"Hakuna zawadi ya maana kuliko zote kwa wazazi wenu ambayo wanafarijika wanapopewa hiyo zawadi,zawadi ambayo mnatakiwa kuwapa wazazi wenu ni ufaulu mzuri kwenye mitihani yenu ya taifa"amesema Mpete
Amesema halmashauri ya mji wa Njombe ina shule nne za sekondari zenye kidato cha tano na cha sita ikiwemo shule ya sekondari Yakobi,Njombe Sekondari (Njoss),shule ya sekondari Uwemba pamoja na Matola shule ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kwenye matokeo ambapo kwa matokea ya mwaka 2024 hazikuweza kuwa na daraja la IV wala 0 na kuwataka kuongeza ufaulu zaidi ya msimu uliopita.
Kwa upande wake duwani wa kata ya Yakobi Michael Uhaula ametoa pongezi kwa mwenyekiti kufika na kutoa hamasa kwa wanafunzi hao huku akibainisha kuwa imani yake ni waanafunzi hao kufanya vizuri kwa kuwa shule yao imekuwa na historia ya matokeo bora.
Nao wanafunzi wa shule hiyo wameshukuru kwa faraja ambayo wamepata na kuahidi kwenda kufanya vizuri kwenye mtihani wao
"Tunashukuru kwa kuja kututia moyo na kutufariji na tunaahidi kupata daraja la kwanza na la pili katika hili tunaamini kabisa hatuwezi kuwaangusha walimu na halmashauri yetu"wamesema Wanafunzi
Post A Comment: