Wizara ya Ujenzi nchini Tanzania katika Mwaka wa Fedha 2025/26 imeliomba Bunge la Tanzania kuidhinisha Jumla ya Shilingi 2,280,195,828,000.00, kwaajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa Miradi ya maendeleo ambapo Takribani Shilingi 2,189,727,558,000.00 zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Wasilisho hilo limewasilishwa leo Jumatatu Mei 05, 2025 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega, akiahidi kuwa kuidhinishwa kwa bajeti hiyo aliyoipa kaulimbiu ya #KazinaUtu, Wizara yake itaendelea kutekeleza miradi ambayo ina manufaa kwa maendeleo ya Nchi kwa kuangazi maeneo yenye uhitaji zaidi sambamba na kuwezesha miundombinu itakayowafanya watanzania waishi maisha ya utu zaidi.

Ameeleza kuwa malengo ya jumla yatakuwa ni pamoja na kujenga barabara za kimkakati zenye kufungua fursa za kiuchumi, kuimarisha shughuli za kijamii sambamba na ujenzi wa barabara zinazounganishwa na njia nyingine za usafiri, Makao makuu ya mikoa, nchi jirani na zile za ulinzi.

Aidha Wizara pia itatekeleza ujenzi wa barabara zitakazokuwa sehemu ya suluhu ya kupunguza msongamano katika Majiji na miji inayokuwa kwa kasi, ukarabati na matengenezo makubwa ya barabara kuu na za mikoa kama sehemu ya kuhakikisha kuwa zinapitika majira yote ya mwaka.

"Tutaimarisha pia usafiri wa miundombinu ya vivuko, miradi ya usalama barabarani ikiwemo ujenzi wa mizani, kujenga nyumba za watumishi wa umma na majengo ya serikali, kuwajengea uwezo wataalamu na Makandarasi wa ndani pamoja na kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vilivyokasimiwa wizara ya Ujenzi."ameongeza kusema.

Katika hatua nyingine pia Waziri Ukega ameahidi kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha zitakazoidhinishwa na Bunge kwaajili ya Wizara yake, akiahidi kuonekana zaidi uwandani (field) kufuatilia kinachoendelea, akitoa pia onyo kwa Makandarasi wote nchini na wale wa kigeni kwamba hatosita kuvunja mikataba yao pale watakapoonekana kuwa na uzembe, ukosefu wa viwango na kupitiliza muda wa kukamilisha miradi bila ya sababu za msingi.

Share To:

Post A Comment: