MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wilayani Arumeru wamedai kuogopa kutembea hadharani wakihofia kupopolewa mawe na wananchi katika maeneo yao ya utawala kufuatia ubovu mkubwa wa barabara katika maeneo hayo uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.


Hayo yameelezwa Mei 7, 2025 na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri hiyo, John Salekwa alipokuwa akizungumzia kero ya barabara ndani ya baraza hilo la madiwani ambapo mbali ya ajenda zingine zilizokuwapo, mjadala mkubwa ulijikita kwenye ubovu wa barabara

" Niwaambieni tu ukweli, huko kwenye kata zetu tukipita tunafunga vioo tunaogopa kupigwa mawe na wananchi kutokana na kero ya barabara na hapa kuna madiwani wanaogopa kupanda hada daladala kwa kuogopa wananachi wao, barabara zetu ni mbovu hazisemeki, Tanzania nzima inajua, "amesema Salekwa.

Amesema ili kukabiliana na hali hiyo Halmashauri hiyo imechukua hatua za haraka ikiwemo kutengeneza vifaa vyake vya kutengeneza barabara na kuwataka madiwani kutafuta fedha kutoka kwa wahisani za kuwekea mafuta pamoja na kununua vifusi na kuvisambaza katika kata zao.

“ Tumehakikisha vifaa vya kuchongea barabara vinakuwa vizima wakati wote, escaveta na shindilia, madiwani njooni mchukue vifaa hivi mkachonge barabara zenu, wewe tu ukipata mfadhili tueleze utapewa magari haya utaenda kutengeneza barabara,”amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Selemani Msumi amesema Halmashauri hiyo imetenga kiasi cha TZS Milioni 45 ambazo zitagawanywa kwenye kata ambapo kila kata itapatiwa TZS 1500,000 kwaajili ya kusaidia kwenye matengenezo ya barabara mbovu.

Amesema fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo kufuatia Tarura kutokuwa na fedha za kutosha za kufanyia matengenezo barabara zote za ndani ya Halmashauri hiyo jambo ambalo limekuwa likisababisha kero kwa wananchi na kwamba fedha zinagawanywa baada ya kukamilika kukusanywa.

Hata hivyo madiwani walihoji uchelewaji wa fedha hizo na kusema wananchi wanazidi kuteseka kwa kukosa huduma za msingi ikiwemo matiababu kufuatia baadhi ya vivuko kusombwa na mafuriko.

Diwani wa kata ya Olturoto Dkt.Baraka Simeone alishauri wakati fedha hizo zikiendelea kukusanywa fedha kidogo iliyopo iendelee kutolewa ili kuondoa usumbufu kwenye maeneo ambayo yamekuwa korofi sana katika kata zao.

Akiahirisha Baraza hilo ambalo pia viongozi mbalimbali wa kisiasa walialikwa akiwemo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo aliwataka madiwani kuwahimiza wananchi kutunza mazingira ili kuepuka athari za mafuriko ambayo yamekuwa yakiendelea wilayani humo.

Amesema uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo kukata miti hovyo, kutupia uchafu kwenye mitaro kwa baadhi ya barabara zilizojengwa wilayani humo, kujenga kwenye njia za maji ni miongoni mwa visababishi vya mafuriko wilayani humo na kupelekea ukaribifu mkubwa wa miundo mbinu ya barabara.


Share To:

Post A Comment: