Angela Msimbira Simanjiro, MANYARA


Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara,Mhe.Fakii Raphael Lulandala ameongoza uzinduzi wa Mradi wa MsingiTek wilayani humo, akitoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia kwa umakini utunzaji na matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA vinavyotolewa na Serikali na Wadau wa Maendeleo.

Akizindua mradi huo leo Mei 7, 2025 katika shule ya msingi Losinyai, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Viongozi hao kuhakikisha vifaa kama vishikwambi vinavyotolewa kupitia mradi wa MsingiTech vinatunzwa ipasavyo na kutumika kama ilivyokusudiwa — kusaidia kujenga Stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa wanafunzi wa madarasa ya awali.


“Ni wajibu wa kila Halmashauri kuhakikisha vifaa hivi havipotei wala kuharibika, bali vinatumika kuongeza ufanisi wa ujifunzaji. Huu ni uwekezaji mkubwa wa Serikali na wadau wake kwa ajili ya kizazi kijacho,” amesisitiza.

Mradi wa MsingiTek unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na shirika la Imagine unalenga shule 500 katika mikoa mitano ya Tanzania Bara. Katika Wilaya ya Simanjiro, shule za msingi zilizohusika katika awamu ya kwanza ni pamoja na Shule ya Msingi Losinyai, Shule ya Msingi Emboreet, na Shule ya Msingi Naisinyai, ambapo wanafunzi wamekabidhiwa vishikwambi vyenye programu maalum za masomo ya awali.

Pia, amezihimiza Halmashauri kuhakikisha zinakuwa na mikakati thabiti ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya unyanyasaji, hasa kwa kuzingatia mazingira ya matumizi ya teknolojia.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa chakula shuleni kama njia ya kupunguza utoro na kuongeza umakini wa wanafunzi darasani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Imagine Tanzania Bi. Jaqline Mgumia amesema shirika hilo linafurahia kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mradi wa MsingiTech, ambao unalenga kuleta mapinduzi chanya katika ujifunzaji kwa watoto wadogo kwa kutumia teknolojia.

“Tumeshuhudia matokeo chanya katika maeneo tuliyofikia. Watoto wanapata hamasa ya kujifunza kupitia michezo ya kielimu kwenye vishikwambi, na walimu nao wamerahisishiwa kazi ya kufundisha,” amesema Bi. Mgumia

Akiwahutubia wanafunzi wa Shule ya Msingi Losinyai, Mhe. Lulandala amewasihi wanafunzi hao kuvitunza vishikwambi walivyopewa, huku akisisitiza kuwa vifaa hivyo ni mali ya Umma na vina thamani kubwa kwa maendeleo yao.





Share To:

Post A Comment: