Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu akizungumza kwenye Mafunzo ya HCD Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya Lotalis Gadau akizungumza kwenye Mafunzo ya HCD Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Imeelezwa kuwa huduma za chanjo husaidia kwa kiwango kikubwa katika kinga kwenye ukuaji wa mtoto hata mtu mzima na kuepuka magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na kuokoa maisha.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu kwenye Mafunzo ya HCD yanayolenga kushirikisha jamii kwa kutumia mbinu Bunifu na Shirikishi katika kutatua changamoto zinazopelekea jamii kuwa na mtazamo hasi kuhusu umuhimu wa huduma za chanjo yanayofanyika katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Aidha, Dkt. Ona ametoa rai kwa wakazi wa Ushetu na Tanzania kwa ujumla kuweka kipaumbele huduma za chanjo hivyo kupitia mafunzo ya “HCD”yatasaidia kuongeza wigo huduma za chanjo.
“Chanjo ina umuhimu mkubwa kwa binadamu hususan kuanzia mtoto mdogo ,mimi mwenyewe mnufaika wa chanjo, kwa hiyo nitoe rai kwa wananchi wa Ushetu kuona umuhimu wa watoto wao kuwapeleka kupata huduma za chanjo kwani chnjo ili mtoto asipate maambukizi mfano Polio, Surua na magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo ”amesema.
Halikadhalika, Dkt. Machangu amesema Wizara ya Afya imeendelea kutoa elimu ya afya kuhusu huduma za chanjo kwa kushirikiana makundi mbalimbali ya kijamii kupitia Mafunzo ya Human Centered Design-HCD ikiwemo makundi ya viongozi wa dini,Tiba Asili, Viongozi wa Sungusungu, pamoja na vipeperushi na umuhimu wa matumizi ya namba 199 kwa ajili ya taarifa sahihi za elimu ya afya.
Akizungumzia madhara ya mtoto endapo hatopata chanjo,Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya Lotalis Gadau amesema kunaweza kusababisha ulemavu wa kudumu ikiwemo kutoona, kupooza au kupoteza maisha.
“Mtoto asipopata chanjo inaweza kupelekea ulemavu wa kudumu, mfano kupooza au upofu au kupoteza maisha”amesema Gadau.
Pia, Gadau amesema ukosefu wa chanjo unaweza kusababisha changamoto ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa Wanawake,hivyo ni muhimu wasichana kupata chanjo hiyo muhimu.
Kwa upande wake Baba Kinara wa Uelimishaji kuhusu umuhimu wa huduma za Chanjo, Ammad Issa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Manispaa ya Tabora amesema alizaliwa mzima baada ya miaka miwili ulitokea ugonjwa wa Surua lakini alichelewa kupata matibabu hali iliyopelekea kuwa na ulemavu wa kudumu wa kutoona huku akitoa wito kwa wazazi kuacha mila potofu kuhusu chanjo.
“Nilizaliwa nikiwa mzima baada ya kufikisha miaka miwili ulitokea ugonjwa wa Surua wazazi wangu wakanipeleka kwa waganga wa Tiba Asili wakifikiri kuwa nimelogwa na hii ilitokana na mimi kukosa chanjo ya Surua, na enzi hizo walifikiri kila ugonjwa umelogwa hivyo nilitafutiwa dawa na kufukizwa na kunyweshwa dawa za kienyeji na baadaye wakanipeleka hospitalini kwa kuchelewa na bahati mbaya nikawa kipofu hadi leo na niwasihi ndugu zangu chanjo zote ni muhimu mimi nilikosa chanjo na sioni mpaka leo hii ”amesisitiza .
..
Ikumbukwe kuwa Mafunzo ya HCD ni mfumo bunifu inayoshirikisha jamii moja kwa moja hadi hatua za mwisho kutatua changamoto katika jamii ili kuwa na uelewa wa pamoja kwenye utatuzi wa changamoto hiyo.
Post A Comment: