Na Denis Chambi, Tanga.

TAFITI zilizokuwa zikifanywa na shirika la Uzikwasa  katika wilaya ya Pangani Mkoani Tanga  zimeendelea  kubadilisha mtazamo hasi kwa wananchi  kuhusu nafasi ya mwanamke na mtoto wa kike katika jamii ambapo wazazi na walezi walikuwa wakikimbilia kuwaozesha na kuwanyima haki yao ya kupata elimu hali ambayo imechangia  kurudisha nyuma wilaya kimaendeleo.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mwanamke yaliyofanyika kiwilaya Msimamizi wa kitengo cha ubunifu na ustawi wa shirika la Uzikwasa Nickson Lutenda amesema kuwa mbali na mtoto wa kike kutokupewa haki ya kielimu kumekuwa na mifumo dume ambayo inamnyima mwanamke kuwa na sauti katika familiya.

"Utafiti wetu tulioufanya mwaka 2015/2016 uligundua mambo makubwa matatatu, kwanza mwanamke Hana sauti katika familiya lakini vilevile mtoto wa kike hapewi nafasi ya kujifunza nafasi kubwa aliyokuwa anapewa ni kuolewa kwa ulazima hata kama mtoto anafanya vizuri darasan anaambiwa ya kwako wewe ni ndoa tu"

"Tuliamua kufanya mafunzo ya uongozi wa mguso kwa jamii ya wilaya ya Pangani kupitia mifumo iliyopo ambayo inamsaidia mwananchi kuweza kupelekea mafunzo katika ngazi ya vijiji, vitongoji mpaka wilaya"

"Tulifanya kazi kwa karibu na kamati za shule, kamati za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto  tuliwapa mafunzo ya namana gani kutambua haki na wajibu wa mtoto   na mwanamke wa Pangani, Uzikwasa tukaja na mpango wa kuwa na chakula mashuleni tuliweza kuhamasisha jamii yenyewe iweze kuchangia chakula tukiamini mwanafunzi akipata chakula shuleni utulivu wake darasani  itakuwa vizuri" alisema Lutenda.

Kufwatia hali hiyo shirika la Uzikwasa kwa kushirikiana na Serikali limeweza kuanziasha  mafunzo mbalimbali yakiwemo ya uongozi  kuanzia ngazi ya vijiji  na kamati za shule  lengo likiwa ni kutambua haki na wajibu wa mtoto hasa wa kike hatua ambayo imeweza kuleta mabadiliko na kuchangia ufaulu mashuleni.

"Baada ya mafunzo yale kila mmoja akaguswa  kuona umuhimu wa elimu kwa watoto hii imeweza kuleta chachu na matokeo  yamekuwa makubwa   hamasa ya wazazi kuweka ulizi kwa watoto imekuwa kubwa matokeo ya darasa la nne , la saba na kidato cha nne Pangani tulikuwa wa mwisho kimakosa lakini sasa hivi tuko nafasi ya tatu na tulishawahi kuongoza na kushika nafasi ya kwanza kimkoa" aliongeza.

Afisa huyo ameiomba Serikali 
 pamoja na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana na shirika la Uzikwasa katika kuendelea kukabiliana  na changamoto mbalimbali  ikiwemo sekta ya elimu maendelo ya kiuchumi kwa wanawake sambana na kupambana vitendo vya ukatili.

"Ombi letu sisi kwa Serikali na jamii kwa ujumla tuendelee kushirikiana  ili kujenga Pangani ya kwetu wote iliyo bora  rasilimali tulizonazo viongozi wetu wanaendelea kupambana na sisi huku katika ngazi ya vijiji , viongozi na wilaya  tuwe na ushirikiano"

Akihitimisha maadhimisho hayo yaliyofanyika katika shule ya msingi Funguni Mkuu wa wilaya ya Pangani Gift Msuya amewataka wazazi na walezi kuzingatia jukumu lao la malezi kwa watoto ili kujenga kizazi Bora cha baadaye huku akiitaka jamii kutokufumbia macho vitendo vya ukatili pale vinavyotokea dhidi ya wanawake na watoto.

"Tuendelee kutambua kwamba siku zote watoto wote wana haki sawa ya kuwezeshwa kwa usawa ili kujenga jamii na familiya yenye usawa katika nyanja mbalimbali,

"Niwapongeze sana taasisi ya  Uzikwasa kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitoa elimu ya ukatili kwa watoto na wanawake  wanafanya kazi nzuri sana katika hili ninaomba  kila mmoja  awe sauti ya mwenzake  ukatili kwenye jamii yetu ya Pangani  haukubaliki tusimame kwa pamoja kila mmoja awe balozi wa mwenzake" alisema Msuya.

Aidha amewataka wanawake kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii hususani mwaka huu Tanzania ikiwa inaelekea kufanya uchaguzi mkuu wa Madiwani wabunge na Rais.

Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri ya wilaya ya Pangani Enock Kirigiti ameeleza  uwepo wa wimbi la watoto wa mtaani ambao wengi wao wametelekezwa na wazazi wao hali ambayo inaweza kuchangia ongezeko la makundi hatarishi kwenye jamii.

"Ofisi ya ustawi wa jamii wilaya ya Pangani inaendelea kuwakubusha wamama kuwa walezi borawa familiya , tunapata wakati mgumu sana ofisi ya ustawi kuhakikisha kwamba watoto mlio walea wanakujua sisi ndio tuwashughulikie  watoto wengi wameingia mtaani kwa sababu unakuta ndoa nyingi zimevunjika , familiya zimewatelekeza ili tuepuke hili janga kina mama tunaombeni mtusaidie sana" alisema Kirigiti.

Maadhimisho ya kimataifa ya siku ya mwanamke  Duniani ambayo hufanyika Kila mwaka ifikapo March 8 mwaka huu kitaifa yanafanyika Mkoani Arusha yakibebwa na kauli mbiu isemayo ' Wanawake na wasichana 2025  tuimarishe haki usawa na uwezeshaji'.


Share To:

Post A Comment: