Na Okuly Julius _ Dodoma
Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMnet) unatarajia kufanya Mkutano wake wa Mwaka wa 9 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha, kuanzia Novemba 4 hadi 7 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 25,2024 jijini Dodoma Rais wa APS-HRMnet ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Xavier Daudi, amesema Mkutano huo utawaleta pamoja mawaziri, makatibu wakuu, wasimamizi wa rasilimali watu, watunga sera, na wataalamu mbalimbali kutoka nchi za Afrika kwa ajili ya kujadili masuala muhimu katika usimamizi wa rasilimali watu katika sekta ya umma.
APS-HRMnet ni mtandao wa wataalamu unaolenga kuimarisha viwango vya kitaaluma na ubora wa huduma za umma barani Afrika,ambayo ilianzishwa mwaka 2009 kufuatia mapendekezo ya Mkutano wa 29 wa Jumuiya ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma wa Afrika (AAPAM) ulioweka msingi wa ushirikiano na ubadilishanaji wa maarifa na mbinu bora katika sekta ya umma.
“APS-HRMnet inajitahidi kujenga sekta ya umma inayowajibika na yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi kwa njia bora na endelevu,” ameeleza Daudi, Rais wa APS-HRMnet.
Daudi amesema mkutano wa mwaka huu, wenye kaulimbiu “Utawala Imara na Ubunifu: Kujenga Sekta ya Umma Yenye Mwelekeo wa Baadaye Kupitia Uongozi wa Rasilimali Watu,” utajadili umuhimu wa kuendeleza uongozi thabiti na uvumbuzi katika utumishi wa umma ili kufikia maendeleo endelevu.
Pia ameeleza kuwa APS-HRMnet inawapa nafasi wataalamu na viongozi katika usimamizi wa rasilimali watu kujifunza na kubadilishana maarifa ya kuboresha sekta ya umma.
Ameelezea malengo makuu ya APS-HRMnet kuwa ni pamoja na kukuza uadilifu na ubora wa kitaaluma katika usimamizi wa rasilimali watu, kushiriki mbinu bora zinazoweza kusaidia mashirika ya umma kuongeza ufanisi, na kutoa zana na data za kuboresha mipango ya usimamizi na maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika.
Aidha, mtandao huo unalenga kusaidia juhudi za kuunda mfumo wa kuthibitisha wataalamu wa rasilimali watu kwa kushirikiana na taasisi za maendeleo ya menejimenti za Afrika na kimataifa.
Amesema mkutano huo pia unalenga kuweka msingi wa ushirikiano na kuhamasisha maendeleo ya kimkakati kwa wasimamizi wa rasilimali watu ili kusaidia nchi wanachama kutekeleza ahadi za umma kama vile Mkataba wa Utumishi wa Umma Afrika.
“Ni fursa muhimu ya kujenga uwezo wa sekta ya umma barani Afrika ili iweze kujibu changamoto na mahitaji ya sasa na ya baadaye,” amesema Daudi.
Daudi ametumia fursa hiyo kama Rais wa APS-HRMnet kuwakaribisha wasimamizi wa rasilimali watu na wadau mbalimbali kutoka kanda zote za Afrika kuhudhuria mkutano huo ili malengo ya mkutano huo yaweze kufikiwa.
Post A Comment: