Katika muendelezo wa hamasa ya wananchi wa Ngorongoro kujiandikisha kuhama kwa hiari, leo tarehe 7 Septemba, 2024 jumla ya kaya 58 zenye wananchi 228 na mifugo 350 wamehama katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera na maeneo mengine waliyochagua katika wilaya za Monduli, Meatu na Simanjiro.
Akitoa taarifa wakati wa kuaga kundi la 19 la awamu ya pili linalohama kutoka hifadhi ya Ngorongoro, Meneja mradi wa kuhamisha wananchi wa Ngorongoro Afisa Uhifadhi Mkuu Flora Assey ameeleza kuwa, kati ya kaya 58 zilizohama leo, kaya 30 zenye watu 151 na mifugo 235 zinahamia Kijiji cha Msomera, Kaya 28 zenye watu 78 na mifugo 115 zinakwenda maeneo mengine waliyochagua katika wilaya za Monduli Mkoani Arusha, Meatu mkoani Simiyu na Simanjiro katika mkoa wa Manyara.
Amebainisha kuwa tangu zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiari lilivyoanza mwezi Juni 2022 hadi kufikia leo Septemba 7, 2024 Jumla ya kaya 1,627 zenye watu 9,778 na mifugo 40,051 zimeshahama ndani ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro.
“Tunawapongeza sana kwa maamuzi ya kuhama hifadhini kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi, maeneo mnayohamia Serikali imeshawajengea huduma muhimu kama shule, zahanati, maji, majosho, mawasiliano, nishati ya umeme, makazi bora pamoja na mashamba ya kilimo na malisho. Pamoja na zoezi hili la kuhama kuendelea, niwahakikishie wananchi ambao bado hawajaamua kuhama kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma za kijamii na katika utekelezaji wa zoezi hili tutaendelea kuzingatia misingi ya sheria, kanuni, taratibu na haki za binaadamu” aliongeza Hamza.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wanaohama kwa hiari, Elizabeth Saiboko kutoka Kijiji cha Nainokanoka amebainisha kuwa ameamua kuhama ndani ya hifadhi ili kuwa huru zaidi na kutafuta kesho iliyobora kwa watoto wake kwa kuwa katika tarafa ya Ngorongoro sheria za uhifadhi zinauiya baadhi ya shughuli za kiuchumi kama kilimo, ujenzi wa nyumba za kudumu, kumiliki vyombo vya moto na uhuru wa kutembea kwa saa 24 tofauti na maeneo mengine nje ya hifadhi.
Post A Comment: