Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) leo tarehe 10 Julai, 2024 wameutambulisha mradi wa 03+(OUR RIGHTS OUR LIVES OUR FUTURE Plus) katika Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA)
Mradi huu umejikita zaidi katika kutoa elimu ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia, mimba zisizotarajiwa, kutokomeza maambulizi ya VVU na magonjwa ya zinaa Pamoja na kutengeneza mazingira salama kwa wafanyakazi na wanafunzi hususani wa Vyuo vya Elimu ya juu na kati
Akimwakilisha Mkuu wa Chuo katika kikao hicho, Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu IAA, Prof. Epaphra Manamba amesema, mradi huo umekuja kwa wakati muafaka na utawasaidia kuwaelemisha wanafunzi kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa ili waweze kufikia malengo waliojiwekea.
“Wanafunzi wanaojiunga na IAA wengi huwa wanakuja wakiwa wadogo sana, wanahitaji kuelemishwa, hivyo kupitia mradi huu watapata Elimu itakayowasaidia kupambana na changamoto za ukuaji wao, ”amesema Prof. Manamba
Mratibu wa Elimu kwa Afya na Ustawi kutoka UNESCO Bw. Mathias Faustine Luhanya amesema Mradi huu unatekelezwa katika Taasisi za Elimu ya juu na kati ili kuimarisha mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia na mpaka Disemba mwakani Vyuo thelathini (30) vitakuwa vimenufaika
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Clement Sanga amesema wizara imekuwa ikishirikiana na UNESCO kupitia mradi huu, ili kuendelea kutokomeza ukatili wa kijinsia vyuoni suala litakalowezesha sekta ya Elimu kubaki katika ubora wake.
Joyce Giovan ni Makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi IAA, ametoa shukrani kwa uongozi wa Chuo na UNESCO kwa kuwaletea mradi huo na kuahidi kutoa ushirikiano na kuhakikisha wanachangamkia fursa hiyo kwa manufaa ya Maisha yao ya sasa na baadaye.
Post A Comment: