Na. Damian Kunambi, Njombe.


Wananchi wa kijiji cha Mundindi ambacho kimetengeneza historia ya kipekee baada ya Serikali ya kijiji hicho kuwakatia bima ya afya wanakijiji wote  Ili kuweza kupata huduma ya afya kwa urahisi pasipo kikwazo cha fedha.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali kulipa fidia ya kupisha miradi ya Liganga na mchuchuma kiasi Cha Sh. Bilioni 15 ambapo serikali ya kijiji hicho kilikuwa na eneo katika mradi Liganga na lililowawezesha kupata fidia kiasi Cha zaidi ya Sh. Milioni 464 ambapo kiasi cha Sh. Milioni 400 kati ya hizo waliamua kununua hati fungani katika moja ya Taasisi ya kifedha hapa nchini.

Akizungumzia fedha hizo mwenyekiti wa kijiji hicho Sapi Mlelwa amesema kiasi hicho Cha Sh. Milioni 400 walichonunua Bondi ya hati fungani kinawawezesha kupata faida ya gawiwo la Sh. Milioni 41 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano hivyo katika gawiwo hili la kwanza wakaona ni vyema kuwakatia wanakijiji wote bima ya afya ambayo imegharimu kiasi cha Sh. 12,930,000.

"Serikali ya kijiji kwa kushirikiana na Diwani wa Kata hii Wise Mgina pamoja na viongozi wengine wa ngazi zote tuliona Kuna haja wananchi wakanufaika moja kwa moja kwa fedha hizi kwa kukatiwa bima ya afya kwakuwa kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu pindi wapatwapo na magonjwa na kupelekea kukutwa na umauti".

Akizindua zoezi la ugawaji wa bima hizo kwa wananchi zaidi ya 2586 wa kijiji hicho, Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amesema kijiji hicho ni kijiji cha mfano kote nchini kwani viongozi wake wamefanya ubunifu Mkubwa sana huku akimuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Stanley Mlay kuhakikisha kuwa kituo cha  afya Cha Kata hiyo hakipungukiwi na dawa Ili wananchi hao waendapo kupata huduma wapate dawa zinazohitaji kulingana na ugonjwa walionao.

"Mganga Mkuu fedha hizi zilizolipwa na kijiji hiki ni fedha nyingi na zinazojitosheleza kununua dawa za aina zote, sasa sitegemei kusikia kuwa wanakijiji hawa wanaishia kupewa Panado tuu badala ya dawa ya ugonjwa husika aliokutwa nao". Amesema Mtaka.

Aidha kwa upande wake kuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amesisitiza kuwa fedha zinazoendelea kupatikana kuwekeza pia katika kuwawezesha vijana kupata elimu ya ufundi itakayo wawezesha kupata ajira katika miradi hiyo mikubwa ya Liganga na mchuchuma pindi itakapo Anza lakini pia kujiajiri wenyewe.

Hata hivyo kwa mujibu wa Diwani wa Kata hiyo Wise Mgina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri amesema suala hilo la kusomesha vijana tayari lipo katika mpango mkakati ambapo wamelenga kuwainua watoto waishio katika mazingira magumu na waliyo yatima kwa kuwasomesha kozi fupi katika vyuo vya ufundi.

Joseph Kamonga ni mbunge wa Jimbo la Ludewa amesema anaona fahari sana kuona fedha fidia alizo zihimiza kwa serikali na Rais kuwezesha upatikanaji wake kwa wananchi hao zimeweza kuleta manufaa makubwa kwao, hivyo anaahidi kwenda kuisisitiza serikali katika upatikanaji wa dawa za uhakika katika hospitali na vituo vyote vya afya Jimboni humo.

" Kwa sasa sina hofu na utoaji huduma katika Kata hii, maana najua mna kituo Cha afya kikubwa na chenye vifaa tiba vya uhakika pamoja na gari ya kubebea wagonjwa hivyo ni matumaini yangu kila kitu kitaenda sawa".

Share To:

Post A Comment: