Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuufungua Mkoa wa Rukwa kwa kujenga na kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja pamoja na Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga.
Dkt. Samia amezungumza hayo Mkoani Rukwa leo Julai 17, 2024 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mandela Wilayani Sumbawanga.
Dkt. Samia ameitaja miradi aliyokagua na kuzindua katika ziara ya siku ya tatu katika Mkoa wa Rukwa kwenye Sekta ya Ujenzi, ikiwemo ufunguzi wa barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port (km 107) kwa kiwango cha lami, uwekaji wa jiwe la msingi ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kaengesa - Chitete (km 6.4) sehemu ya Kaengesa Seminari.
“Rukwa tunaifungua kwa njia zote, tunaifungua kwa barabara, tunaifungua kwa usafiri wa kwenye maziwa na tunaifungua kwa anga”, amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga port (km 107) kwa kiwango cha lami itasaidia kupunguza msongamano wa malori katika eneo la Tunduma Mkoani Songwe.
Aidha, Dkt. Samia amemuelekeza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuunganisha barabara ya lami ya Kaengesha - Seminarina na barabara zinazozunguka shule ya Seminari ya Kaengesha ili kuweka sura nzuri ya Shule hiyo.
“Shule ya Seminari ya Kiengesa ni ya heshima sana na pale ndipo pametoa Mhashamu Askofu Cardinali Polycarp Pengo, Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda na Waheshimiwa Wabunge wa sasa wa Jimbo la Kwela na Nkasi Kusini Waheshimiwa Deusi Sangu na Vicent Mbogo”, amefafanua Rais Dkt. Samia.
Vilevile, Dkt. Samia ameeleza kuwa uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga unaoendelea kutekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Rukwa utaleta huduma nyingi na bora kwa wana Rukwa.
Post A Comment: