Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari, leo Juni 26, 2024, amesifu uwepo wa hoja chache za za kiukaguzi kupitia kwa Mdhibiti na Mkaguzo Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG).
Bi. Judica Omari, amesema hayo, wakati akizungumza katika Kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, baada ya kuwasilishwa na kujadiliwa kwa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
“Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete mmekuwa na ushirikiano mzuri katika Utendaji kazi wenu, ndio maana hata hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali zimekuwa chache, naamini mwaka Fedha ujao mtaweza kuzimaliza kabisa” Alisem Bi. Judica.
Aidha, amesema kuwa, lengo la serikali ni kukusanya Mapato ambayo yatatumika katika kuleta maendeleo nchini, pamoja na kuboresha utolewaji wa huduma mbalimbali za kijamii, ambapo ameziagiza Halmashauri zote mkoani Njombe, kusimamia makusanyo hayo kiufasaha.
Sambamba na hayo, amewasihi madiwani kushirikiana na Idara ya Ardhi kuhakikisha kuwa wanakuwa chachu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, kutokana na kuwepo wa changamoto hiyo kwenye maeneo mengi, pamoja na kusimamia sheria za Ardhi ipasavyo.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Makete, Ndg. Clemence Ngajilo, amewashukuru watumishi wa Halmashauri kwa utendaji kazi bora, na kuwataka kuendelea hivyo ili Wilaya ya Makete iweze kukua kiuchumi.
Nae, mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Mhe. Christopher Fungo, ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa fedha kiasi cha Shilingi bilioni 1.709,100,000/= kwaajili ya kuboresha Elimu Msingi na Sekondari.
Ikumbukwe kuwa, Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani, kimeketi leo Juni 26,2024 katika ukumbi wa mikutano wa Bomani, uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete, ikiwa ni kikao maalum cha Kujadili taarifa ya Mdhibigi na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Post A Comment: