Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan imeendelea kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara na wawekezaji Sekta ya Utalii ili kuwarahisishia ufanyaji biashara na kuendelea kuikuza Sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelllah Kairuki mara baada ya kufungua rasmi Maonesho ya Kimataifa ya Kili-fair  Juni 7,2024 jijini Arusha.

“Tunaendelea kumshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuwa ameendelea kuhakikisha kunakuwa na vivutio mbalimbali vya utalii katika ufanyaji wa biashara na vya kikodi kwa ajili wa wawekezaji hasa katika sekta yetu ya utalii” Mhe. Kairuki amesisitiza na kuongeza kuwa  juhudi hizo za Mhe. Rais zimesaidia kuongezeka kwa makusanyo ya mapato pamoja  na idadi ya watalii nchini.

Aidha, amesema maonesho hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa mwaka 2024 kwa kuwa na waonyeshaji  zaidi ya 460 ambao wametoka nchi takribani ukilinganisha na mwaka jana ambapo walipata waonyeshaji 400 tu.

Amesema maonesho hayo ya siku tatu yanawakutanisha wadau wote wa sekta ya utalii kutoka Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na pamoja na Nchi za nje ambapo wapo waonyeshaji kutoka Sekta za hoteli,  ukarimu, migahawa na mahema kwa ajili ya hifadhini,magari yanayotumika katika hifadhi na huduma mbalimbali. 

Pia amesema kuwa yamekuwa ni maonyesho yenye tija lakini kwa Sekta binafsi,Taasisi za Serikali, Zanzibar, Taasisi za TTB, kamesheni ya utalii ya Zanzibar na taasisi zote za pande zote mbili za muungano ambao wameshiriki ili kutoa ufafanizi mbalimbali  kadri unavyohitajika kwa wadau wa utalii.

Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Malikale Zanzibar, Mhe. Mudrik Soraga amesema kuwa kuna haja ya kuendeleza na kuwa na mkakati mzuri wa mawasiliano ambao utakuwa unaweza kutoa taarifa kwa mgeni na kuweza kuona kwamba anapokuja Zanzibar anaweza kuja Arusha ama anapokuja Arusha anaweza kwenda Zanzibar.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaahidi itaendelea kushiriki katika matukio makubwa ya kutangaza utalii kama hayo kwa sababu inaleta hamasa kwa sekta ya utalii kwa pande zote mbili.

Naye Mkurugenzi wa Kilifair Promotion Company Ltd na mwaandaaji wa tamasha la Kilifair, Dominic Shoo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau wote wa utalii wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika maonesho hayo ili kuweza kujifunza na kujionea masuala mbalimbali ya Sekta ya Utalii

Share To:

Post A Comment: