Kulia ni mkuu wa wilaya ya Njombe Mhe.Kissa Kasongwa akipokea mwenge wa uhuru toka kwa Mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe Mhe.Claudia Kitta

Maria Mapunda Mmoja wa wakimbiza mwenge wa uhuru Kitaifa akipaka rangi bweni la shule ya sekondari Sovi Halmashauri ya wilaya ya Njombe.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2024 Godfrey Mnzava amezitaka kamati   za watumia maji CBWSO wilayani Njombe kuendesha miradi ya maji kwa usawa na sio kutoa huduma kwa upendeleo.

Mnzava ametoa agizo hilo akiwa katika kijiji cha Nyombo Halmashauri ya wilaya ya Njombe baada ya kuzindua jumuiya Nne za watumia maji ambapo amesema azma ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama bila upendeleo na hivyo viongozi wanapaswa kufanyakazi kwa weledi.

Awali Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amesema Mwenge wa Uhuru umetembelea umekagua na kuzindua miradi 5 yenye thamani ya Zaidi ya shilingi Milioni 146 katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoani Njombe.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Njombe Elikalia Malisa Amesema jumuiya hizo zitakwenda kusimamia miradi ya maji ili iweze kujiendesha na kutoa huduma vizuri kwa wananchi.

Mbunge wa jimbo la Lupembe Edwin Swalle amesema Serikali imepeleka miradi mingi  katika jimbo hilo jambo ambalo limechagiza kwa kiasi kikubwa maendeleo kwa wananchi.

Baadhi ya wananchi wa Nyombo na viongozi wa kamati za maji wamesema miradi hiyo imekuwa msaada mkubwa kwani maji yanapatikana kwa uhakika.

Aidha Mwenge wa uhuru ukiwa katika eneo la Mkesha huko Mtwango umekutana na Tume ya Ushindani ya biashara FCC ambapo Mkuu wa Tume hiyo Kanda ya Nyanda za juu kusini Dickson Mbanga amesema baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu wamekuwa wakijihusisha kuingiza na kuuza bidhaa feki jambo ambalo hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa huku kiongozi wa mbio za mwenge akiagiza kuongezwa kwa nguvu ya utoaji elimu juu ya bidhaa halisi na bandia.

Mwenge wa uhuru umekesha Lunguya Mtwango na Kisha utakabidhiwa Katika Halmashauri ya Mji wa Makambako juni 21 mwaka huu.

Share To:

Post A Comment: