Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro 

Kufuatia changamoto za milipuko ya mitambo ambazo zimekuwa zikivikumba baadhi ya viwanda nchini na kusababisha vifo,kumewaibua baadhi ya wananchi waishio Kata ya Arusha Chini wilayani Moshi Mkoani kilimanjaro kukusanyika kukiombea Kiwanda cha sukari cha TPC kuelekea mwaka mpya wa uzalishaji 2024/2025 unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.


Mlipuko katika Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa Morogoro, Mnamo Mei 23, 2024 kulikotokea mripuko huo uliosababishwa na hitilafu ya umeme ambayo ilisababisha bomba la mvuke kupasuka na kusababisha majeruhi na vifo vya watu 11 umekuwa chachu ya wanavijiji hao kukutana na kuombea kiwanda cha Sukari TPC..


Wananchi hao wa vijiji zaidi ya nane vikiwemo vijiji vya Newland,Mserikia,Kikavu,Msitu wa Tembo,Londoto,Chemichemi,Kiungi, na Shabaha vilivyopo katika Kata hiyo pamoja na vijiji vingine  jirani vinavyozunguka kiwanda hicho wamekusanyika kushukuru,pia kumuomba Mungu awasimamie katika mwaka mpya wa uzalishaji.

Kusanyiko hilo ambalo limejumuisha waumini na viongozi mbalimbali wa kampuni,dini na serikali,limefanyika leo katika uwanja wa mpira wa Limpopo uliopo kiwandani hapo lengo likiwa ni kuombea amani,utendaji mzuri,uongozi,wafanyakazi,pamoja na mitambo ya uzalishaji isilete madhara kwao ikiwemo miripuko.


Wananchi hao wamesema wamekuwa wakifanya hivyo kila mwaka lengo likiwa ni kumshirikisha Mungu katika utendaji kazi wa kiwanda hicho ili akiepushe na madhara ama ajali zinazoweza kuleta hasara na kupoteza maisha ya watu kiwandani hapo kama ambavyo imetokea Kwa kiwanda cha Sukari Cha Mtibwa.


Mkazi wa kijiji cha Kikavu,Christina Mgonja amesema "Ni faraja kubwa kuona uongozi wa kiwanda hiki kushirikisha wananchi kukiombea hasa kinapokwenda kuanza uzalishaji wiki hii baada ya kusimama kwa miezi mitatu kuzalisha sukari sasa tunaanza na maombi kwani kimendelea kutoa mchango muhimu kwa jamii yetu na kukuza uchumi na maendeleo ya mkoa wa Kilimanjaro".

Mkazi wa kijiji cha Bwawani,Moshi Mgimwa yeye ameomba jambo hilo liwe endelevu kwani limekuwa la baraka na linawapa moyo kuanza kazi kwa moyo mkuu kwani dunia sasahivi imejaa majanga mengi huku akitolea mfano mlipuko wa bomba la kiwanda cha Sukari Cha Mtibwa.


Wakati huohuo mmoja wa wafanyakazi kiwandani hapo kitengo cha fedha na stoo,Sarah Mroki amesema wanakumbana na changamoto nyingi wakiwa kiwandani hapo ikiwemo mitambo kulipuka,shoti za umeme na uchumi kushuka hivyo kuanza na maombi kutaimarisha hayo yote na kufanya kiwanda kuwa imara.


Akihubiri katika kusanyiko hilo,Joseph Moshi ambaye ni mchungaji wa kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) Arusha Chini amesema wameandaa kusanyiko hilo kuomba Mungu awaepushe na ajali za moto,wafanyakazi wawe na afya njema pamoja na kuimarisha uzalishaji mzuri na bora kiwandani hapo.


Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu Utawala wa TPC, Jaffary Ally amesema kusanyiko hilo la kiungwana lilipitishwa na kikao cha bodi ya kiwanda hicho kwamba viongozi wa dini na waumini mbalimbali wa eneo hilo wana wajibu kushiriki katika kumuomba Mungu kuiombea kampuni,wafanyakazi wao,menejimenti yao lakini kuiombea jamii inayoishi ndani ya kiwanda hicho.

Amesema sekta ya sukari nchini imekumbwa na majanga ya mlipuko ambapo hivi karibuni bomba la kiwada cha Sukari cha Mtibwa lililipuka na kupoteza uhai wa watu 11 papo hapo kama ilivyo tokea kwa kiwanda cha TPC miezi kadhaa iliyopita.


"Yaliyotokea Mtibwa ni kama yale yale yaliyotokea tarehe 18 mwezi wa 12 hapa TPC.Bomba linalobeba stimu lilikuwa bomba bora lilipasuka.Ndani walikuwepo Mainjinia na Wataalamu mbalimbali lakini Mungu alipanga yake.Bomba lile lilipasuka basi wenzetu 11 waliopoteza maisha pale pale na wengine wawili walienda kupoteza maisha walipofika hospitalini" amesema Ally.


Naye Afisa Sheria na Uhusiano wa kiwanda hicho,Abdulkadir Mohamed (wakili) amesema mbali na kusanyiko hilo pia wamekuwa wakishishikiana na Shirika lisilo la kiserikali la FT Kilimanjaro kuchukua jukumu la kujenga ushirikiano na wananchi hasa katika sekta nne (Elimu, Afya, Kipato, Miundombinu) ambazo zinaunganishwa pamoja kusaidia jamii ya watu wa Kilimanjaro.


 

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: