Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka wananchi wa jimbo hilo kuacha siasa za malumbano kwani hazileti maendeleo na badala yake wajikite katika kujiletea maendeleo.

Dkt.Biteko ameyasema hayo  wilayani Bukombe Mkoa wa Geita wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bukombe kwa mualiko wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita katika  mkutano uliolenga  kutathmini hali ya maendeleo kwenye jimbo hilo.

Dkt. Biteko amesema Wana Bukombe hawana mtu mwingine wa kuwaletea maendeleo isipokuwa wao wenyewe na kuongeza kuwa siasa za malumbano hazileti maendeleo bali zinayachelewesha hivyo amewasisitiza  wananchi hao kufanya kazi kwa bidii.

Aidha,  kuhusu  uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt. Biteko amewahimiza Wananchi wa jimbo hilo kuchagua viongozi wanaofaa  na wanaotokana na CCM  ili kutocheleweshewa maendeleo na kuwaasa kuwa  wajifunze kuushinda ubaya kwa wema.

Akizungumzia miradi ya maendeleo jimboni Bukombe Dkt. Biteko amesema ‘’napenda nimpongeze Mhe Rais kwa kutuletea fedha za kutosha takribani shilingi bilioni 79 katika mwaka mmoja tu kwa ajili ya maendeleo Wilaya ya Bukombe kwenye sekta ya Elimu, Afya pamoja na  miradi mingine ya maendeleo."

Ameongeza kuwa,  mwaka 2015 Wilaya ya  Bukombe ilikuwa na vituo vya afya viwili na zahanati 4, mtandao wa barabara  ulikuwa kilomita 256 tu, mtandao wa maji wilaya nzima ulikuwa chini ya asilimia 15  na  hakukuwa na  sekondari kwenye kata lakini sasa  kuna shule mpya za sekondari 7, shule za msingi mpya 11, vituo vya kutolea huduma za afya  25 na mtandao wa barabara umefikia  kilomita 1400 hivyo amewataka wananchi kutembea kifua mbele  kwa maendeleo yaliyopo.

Kuhusu siasa amesema ‘’mnapofanya siasa msing’oe Bendera za chama  kingine cha siasa na  inapotokea kuna mtu anang’oa bendera zenu niambieni nitanunua nyingine, kwani bendera haipigi kura, haichagui wala haiombi kura bali ni kitambulisho kuwa hiki chama kipo hivyo hakuna sababu ya kuvunja undugu kwasababu ya vyama vya siasa kwani sisi sote ni ndugu."

Kwa upande wake Naibu Waziri katika  Ofisi ya Rais- TAMISEMI,  Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka matokeo zaidi kuliko maneno na ndio maana ameagiza TAMISEMI kuhakikisha inakarabati miundombinu iliyoharibiwa na mvua  na kuhakikisha watumishi wa Sekta ya Afya na Walimu wanapelekwa  wilayani Bukombe kwa maslahi mapana ya wananchi pamoja na  kuboresha maendeleo.

‘’Wananchi wa Bukombe mna bahati ya kuwa na kiongozi mchapakazi, mpenda maendeleo na mwenye kiu ya kuleta maendeleo hivyo mumuenzi kwa vitendo’." Amesema Mhe. Dugange

Mkutano huo wa hadhara ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Geita Mhe. Rose Busiga na Wenyeviti wa CCM Mkoa na Wilaya.

Share To:

Post A Comment: